Pacoume ainusuru Yanga kufungwa na Al Ahly

Na Badrudin Yahaya

MABINGWA wa soka nchini Tanzania, Klabu ya Yanga, imebanwa mbavu nyumbani kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.Mchezo huo wa Kundi D uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ulishudiwa timu hizo zikienda mapumziko matokeo yakiwa 0-0.

Kipindi cha pili, dakika ya 87 ya mchezo mshambuliaji wa Al Ahly raia wa Afrika Kusini, Percy Tau aliipa timu yake bao la uongozi baada ya walinzi wa Yanga kushindwa kuokoa mpira ambao ulikuwa katika eneo lao la hatari.

Hata hivyo bao hilo halikudumu kwa muda mrefu kwani dakika ya 90, kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua aliisawazishia timu yake kwa bao safi baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Al Ahly, Mohamed El Shenawy akiwa ndani ya boksi.

Kwa matokeo hayo, Yanga sasa wanakuwa wamevuna alama 1 baada ya kushuka dimbani mara mbili huku Al Ahly akikwea kileleni baada ya kufikisha alama 4.

Katika dakika 90 za mchezo huo, kila timu ilipoteza nafasi za wazi zaidi ya mbili kutokana na makipa wa kila upande kuokoa mabao ya wazi.

Wachezaji Clement Mzize na Kennedy Musonda kama wangekuwa makini wangekwamisha mpira wavuni kwani kwa nyakati tofauti walikutana ana kwa na El Shenawy lakini kipa huyo alipangua.Lakini Mohamed Kaharba na Tau kama wangetulia wangeifungia Al Ahly mabao lakini uhodari wa Kipa, Djigui Diarra uliwafanya mashuti yao yatue katika mikono ya kipa huyo.

Timu za Medeama na CR Belouizdad ambazo zilicheza Ijumaa zenyewe zina alama tatu kila mmoja.

Mchezo unaofuata kwa Yanga kwenye michuano hiyo utakuwa ni dhidi ya Medeama FC na baada ya hapo michuano itasimama kupisha michuano ya AFCON 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *