Na Mwandishi Wetu
OFISA Tarafa wa Kata ya Kariakoo, Adrina Kishe, amesema onesho la Za Kwetu Eco Fashion Show ni moja la onesho linalofundisha jamii kuwa na uwezo wa kubuni bunifu mbalimbali kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo nchini ambazo zina ubora.
Amesema onesho hilo limekuwa na tija kwa wabunifu na wanamitindo kujifunza ni namna gani wanaweza kubuni bunifu zenye kuleta tija kupitia mitindo.
Akizungumza hayo juzi jijini Dar es Salaam katika onesho hilo, Kishe amesema serikali itaendelea kuunga mkono miradi mbalimbali inayobuniwa na wabunifu kama hiyo ya kimitindo ambayo inaleta tija siyo tu kwa wabunifu bali kwa jamii nzima.

Ametoa wito kwa wabunifu na wanamitindo kuendelea kutumia majukwaa yao ya fashion show kuhamasisha matumizi ya bidhaa rafiki kwa mazingira na kuzalisha bidhaa zinazoheshimu utamaduni wa kitanzania.
”Za Kwetu Eco Fashion Show siyo tu maonesho ya mitindo bali ni jukwaa linaloonyesha uzalendo na uwajibikaji wa kijamii, tumeshuhudia vipaji mbalimbali vya wabunifu wetu wakitumia malighafi za asili na za kirafiki kwa mazingira.
Awali akizungumza katika onesho hilo wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Shirika la Ladies Joint Forum (LJF) ambao ndio waratibu wa Fashion show hiyo ya ‘Za Kwetu Eco Fashion Show’, Fransisca Mboya, amesema onesho hilo limeandaliwa kwa dhamira ya kukuza ubunifu, kulinda mazingira na kuimarisha uchumi wa kijani kupitia sekta ya mitindo.
Amesema LJF kama waandaaji wakuu wa onesho hilo wanaamini kwamba wanawake ni nguzo muhimu katika juhudi za maendeleo endelevu.

Amesema kupitia ubunifu wa kijana jamii inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga mustakabali bora kwa kizazi kijacho.
Pia Mwenyekiti wa Kamati ya onesho hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisis ya Environmental Conservation Community of Tanzania (ECCT), Lucky Michael, amesema onesho hilo limekuwa la mafanikio makubwa kwa sababu ya ushirikiano kati ya wao na serikali.