Na BBC, Nairobi
NI takribani miaka sita sasa imepita tangu Nkatha Mwenda anywe pombe na kuvuta sigara kwa mara ya mwisho.
Nkatha Mwenda kutoka Nairobi nchni Kenya, anasema ni jambo ambalo anajivunia na kulifurahia sana.
Anakumbuka jinsi alivyoanza kujikuta katika hali ya kupenda kunywa kupita kiasi mwanzoni mwa mwaka 2000, ni mara tu baada ya kumaliza shule ya sekondari na kuingia chuo cha mafunzo ya rubani hapa Nairobi.
“Nilikuwa bado binti mwenye ndoto nyingi, nilijiona kuwa rubani wa kimataifa siku moja,” anasema Nkatha
Nkatha alisomea urubani kwa kipindi cha mwaka mmoja, ikiwa ni masomo ya kwanza yanayohitajika kwa kila rubani kuwa na leseni ya kurusha ndege mwenyewe hewani, aidha anakiri kwamba ndio kipindi hicho alianza kujifunza matumizi ya pombe na sigara.
Anasema wakati anajifunza kuwa rubani alikutana na marafiki ambao walikuwa wanapenda sana vileo baada ya masomo.
Licha ya kufaulu hatua ya kwanza ya urubani, alihitaji Nkatha alifaulu na cheti cha kwanza cha kuwa rubani binafsi, ila alihitajika kwenda kwenye masomo mengine ya urubani ili kuanza kazi rasmi.
Wazazi walipata changamoto ya kumlipia ada, ambayo ilikuwa ghali kwa mtu kusomea urubani. Hivyo ilibidi wamwambie ajiunge na chuo kikuu kimoja nchini Kenya asomee somo la lishe bora, jambo ambalo Nkatha hakuridhishwa na uamuzi uliyochukuliwa na wazazi wake, akilini mwake alikuwa amejitayarisha kuwa rubani tu.
“Nilipogundua kwamba sitaendelea na masomo ya urubani hapo ndipo uraibu wa pombe uliniingia kabisa, nilificha uchungu wa kukosa kuwa rubani kwa kunywa pombe, nilianza kuwa na sonona na msongo wa mawazo baada ya kugundua kuwa ndoto yangu ya kuwa rubani imekufa tayari.”
Nkatha anasema kwamba hali ya uraibu iliongezeka wakati anaingia chuo kikuu, kwani alishindwa kukubali mabadiliko na hatma ya kuwa hangeweza kuwa rubani tena hivyo aligeukia pombe na sigara japo aliendelea na masomo lakini muda wake mwingi ulipotea kwenye ulevi.
Baada ya kuhitimu elimu yake ya juu, Nkitha anasema alibahatika kuwa mjanja wa kutafuta kazi, licha ya kuwa alikuwa na shida ya unywaji wa pombe alifaulu vizuri na kuwa mtaalam wa lishe bora alifanikiwa kupata kazi mara tu baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu.
Ila alipoajiriwa ndio kama ulizidisha ile kiu ya kunywa pombe na uvutaji wa sigara.
“Ninapoangalia nyuma ninaona nilikuwa nachukua maamuzi ambayo yalikuwa na madhara makubwa katika maisha yangu, siku ya kwanza niliyoajiriwa kazi nilifika ofisini nikiwa nimelewa chakari, ni mwenzangu mmoja aliyenisitiri na kunishauri nielekee sehemu maalum kulala ili kuaondoa harufu ya pombe na ulevi kichwani,” anakumbuka Nkatha.
Aibu ya Pombe
Na kwa miaka 10 baada ya kuajiriwa kazi Nkatha alijikuta akinywa pombe kupindukia, anasema kwamba kuna wakati alikunya pombe Jumatatu hadi Jumapili bila kujali chochote.
Madhara ya unywaji huu wa pombe yalianza.
Cha kwanza anasema kuwa kila wakati alikuwa anajikuta amezimia kwa kunywa sana au amelala sehemu ambayo haijui au hakumbuki ni vipi alifika nyumbani. Vile vile anasema kwamba alinusurika mara kadhaa na ajali mbaya za barabarani kwani alikuwa anaendesha gari lake akiwa amelewa.
Vilevile nafasi yake kazini ilimuwezesha kusafiri nchi mbalimbali na maeneo mbalimbali nchini Kenya akiwafundisha watu kuhusu masuala ya kampuni anayofanyia kazi, wakati mwingine anasema alikuwa mlevi na sio mara moja au mbili alishindwa kuingia kwenye mikutano mikubwa kwasababu ya kulewa hivyo alikuwa akishindwa kusimama kwenye majukwaa kutoa hotuba za kikazi.
Matukio kama haya ya aibu na fedheha anasema yalianza kumtia wasiwasi kwani watu waliokuwa karibu na yeye walikuwa wamegundua kuwa alikuwa na shida ya unywaji hatari wa pombe, Nkatha anasema kimoyomoyo alitamani aache kabisa pombe na sigara ila hakuwa na nguvu kabisa ya kuhimili kuacha.
Kuacha kunywa pombe
Anakumbuka mwaka 2016 disemba wakati wa msimu wa sikukuu za krismasi na kama kawaida yake alikuwa tayari kusherehekea kwa mbwembwe za kila aina hasa katika unywaji, ila anasema baada ya usiku mmoja wa kunywa pombe, aliporejea nyumbani na kulala alipata ndoto, anasimulia kuwa katika ndoto hiyo alijiona akiwa kwenye ajali mbaya sana ya barabarani na kwamba alifariki kutokana na ulevi uliomsababisha kutodhibiti gari lake.
Nkatha alipoamka kutoka usingizini anasema alihisi uoga na wasiwasi kuwa huenda ndoto hio ikatimia iwapo ataendelea na unywaji pombe anakumbuka Disemba 24 mwaka 2016 ndio ikawa siku aliyoacha uraibu wa pombe na sigara.
Nkatha anasema kwamba imemgharimu msimamo dhabiti wa kuwa harudi nyuma katika maisha ya kale ya pombe. Vilevile kichochezi kikubwa chake anasema kwamba ilikuwa kuandamana na marafiki ambao walikuwa walevi ilibidi aachane nao.
Mwisho wa uraibu wa unywaji pombe na matumizi ya kuvuta sigara Nkatha alipata maono mapya ya kuanza shirika lisilo la kiserikali linalohamasisha wanawake kupambana dhidi ya matumizi ya pombe na dawa ya kulevya. Nkatha anasema kwamba katika vitongoji vya eneo la Ruiru Kaunti ya Kiambu aliwakusanya wanawake waliokuwa wanajiuza miili yao ambao walikuwa wametekwa katika uraibu kama yeye na kuwasaidia kujielewa na kuacha tabia hiyo.
Shirika lake kwa jina ‘Grace Youth Recovery Center’ linahusika sana na harakati dhidi ya unywaji pombe kiholela.
Nkatha anasema kwamba miaka 10 ambayo alikuwa mateka wa pombe lilikuwa ni somo kubwa kwake na amechukua jukumu la kufanyakazi na wanawake wanaojikuta kwenye uraibu wa pombe kwani anaelewa kuwa baadhi ya wanawake hao wanaotumia pombe vibaya huwa ni sonona na taabu nyingi ambazo zinawakumba kupitia unywaji huo wa kiholela.