Nje, ndani yaliyojiri Mkutano Mkuu TFF

Na Asha Kigundula, Tanga

MKUTANO Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), umemthibitisha Wallace Karia kuwa Rais wa shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo mwishoni mwa wiki mkoani hapa.

Hatua hiyo imetokana na kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, hivyo wajumbe wote 76 waliokuwa na sifa ya kupiga kura walinyosha mikono kumthibitisha kwa wadhifa huo hadi mwaka 2029.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kiomoni Kibamba, amewajulisha wajumbe kuwa kwa vile Karia alikuwa mgombea pekee angepewa dakika za kujieleza kisha mkutano umthibitishe.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, alisimama na kutoa hoja ya kutaka athibitishwe kwanza na kama ana maelezo atasema baada ya kuthibitishwa, kauli ambayo iliungwa mkono na wajumbe wote.

Wajumbe wa mkutano huo wamempitisha kwa kishindo Rais Karia, baada ya kumpigia kura za ndiyo kwa asilimia 100.

Karia alikuwa mgombea pekee wa nafasi ya urais kutokana na wagombea wengine kuenguliwa na Kamati ya Uchaguzi kwa kushindwa kutimiza vigezo vya kikanuni.

Rais wa TFF, Wallace Karia

Kwa ushindi huo, Karia anaendelea kuiongoza TFF katika muhula mpya, huku wajumbe wakionesha imani kubwa kwake katika kuendeleza maendeleo ya soka la Tanzania.

Katika hatua nyingine, Rais Karia amemteua tena Athumani Nyamlani kuwa Makamu wa Kwanza wa rais wa shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Rais anateua wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji ambao wanathibitishwa na Mkutano Mkuu wa TFF na miongoni mwa wajumbe hao anatoka Makamu wa Kwanza wa Rais.

Nyamlani ametangazwa juzi kushika wadhifa huo kwenye mkutano huo ikiwa ni awamu ya pili, ambapo mara ya kwanza aliteuliwa mwaka 2021. 

Lugano ambwaga Nyambaya

Katika Uchaguzi wa Kanda Maalum kinyang’anyilo kikali kilikuwa cha Kanda namba moja, ambacho kiliwakutanisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Namungo, Hosea Lugano.

Mnyukano ulikuwa mkali huku Nyambaya akiangukia pua baada ya kupata kura 33 dhidi ya 38 za mpinzani wake, Lugano.

Mwenyekiti mpya wa DRFA, Hosea Lugano

Wengine walioibuka washindi ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Salum Kulunge dhidi ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mwanza, Vedastus Lugano na James Mhagama akimshinda Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Cripyan Kuyava huku wajumbe watatu, Mohamed Aden, Mwisho Bukuku na Khalid Abeid wakipitishwa na mkutano mkuu kutokana na kutokuwa na wapinzani.

Wajumbe hao wameungana na wajumbe wengine wanne ambao wameteuliwa na Rais wa TFF katika Kamati ya Utendaji ambao ni Somoe Ng’itu, Evans Mkeusa, Azam Muft na Debora Mkemwa. 

Uchaguzi huo ulivutia wadau wengi baada ya kuendeshwa kiweledi huku kila mjumbe akishuhudia kila aina ya tukio ikiwa pamoja na uhesabuji wa kura. 

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Karia alisema yeye na kamati yake wataendelea kusimamia sera ya mabadiliko katika uendeshaji mpira wa miguu.

Amesema anajivunia kuona vikosi vya timu za Taifa vinafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kama ilivyo sasa kwa timu ya Taifa imeingia hatua ya robo fainali bila ya kufungwa na inaongoza kundi.

Yanga haijapiga kura

Klabu Yanga ni miongozi mwa wajumbe 7 walioshindwa kupiga kura kwenye uchaguzi huo baada ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said kutuma mwakilishi badala ya kuja mwenyewe.

Hivyo mwakilishi huyo aliondolewa kuwa miongoni mwa wapiga kura ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi alisema katika kupiga kura wanaopiga ni wahusika na si wawakilishi.

Wengine waliokosa kupiga kura ni pamoja na Mwakilishi Mkoa wa Lindi na chama cha makocha ambao hao sababu ni kushindwa kufanya uchaguzi wao binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *