Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Airplanes Africa Limited (AAL) yenye makao yake Morogoro, imetangaza ndege tatu za kwanza zilizotengenezwa Tanzania, zinazojulikana kama Skyleader 600, zimeanza rasmi safari zake ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa AAL, David Grolig, ndege moja kati ya hizo tatu imetua kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa kuanza kufanya kazi.
Grolig alithibitisha kampuni yao imepata kibali kwa mamlaka husika ya masuala ya usafiri wa anga na hiyo imefanyika baada ya kuthibitishwa ubora wake.
Alisisitiza Ndege ya Skyleader 600 ni ya kisasa, ina ubora wa hali ya juu na inakidhi viwango vyote vya kimataifa na kuruhusiwa kuanza kufanya kazi.
“Tumetengeneza ndege tatu aina ya Skyleader 600 hapa Tanzania, na sasa ziko tayari kuuzwa. Ndege hizi zinatoa suluhisho bora la usafiri kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, na tunakaribisha wateja wanaopenda kumiliki,” alisema Grolig.
Alisema uamuzi wa kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa ndege nyepesi Tanzania ulitokana na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na utayari wa wananchi kukubali teknolojia na kujifunza ujuzi mpya.
Alisema ndege hiyo inabeba abiria wawili, pamoja na rubani na inafaa kwa wasafiri wa kibiashara wanaofanya safari za umbali mrefu.
“Tulifanya utafiti wa kina kuhusu mahitaji ya wasafiri wa kibiashara ambao mara kwa mara husafiri kwa umbali mrefu. Kutokana na utafiti huo, tulitengeneza ndege ambayo inawawezesha wafanyabiashara kusafiri kwa ufanisi na kuhudhuria mikutano mbalimbali nje ya maeneo yao kabla ya kurejea mjini,” alisema.
Aliongeza kwa kusema gharama za kununua ndege hizo ni nafuu kama kumiliki gari.
“Mafanikio ya mradi huu yanatokana na jitihada za pamoja na za kujituma za timu yetu ya Kitanzania na Jamhuri ya Czech,” alisema Grolig.
Ndege hiyo ilioneshwa hivi karibuni katika Maonyesho ya Watengenezaji wa Bidhaa ya Tanzania (TIMEXPO 2024) yanayoendelea katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).