Na Badrudin Yahaya
MFUKO wa Misitu Tanzania (TaFF), umetangaza kutoa ruzuku ya shilingi milioni 402 kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambazo zitatumika kupanda miti ya mpira kwenye shamba la ukubwa wa hekta 402, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kuingia mkataba huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt. Tuli Msuya amesema lengo la kutoa ruzuku hiyo ni kuendeleza kilimo cha miti ya mpira katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya kilimo endelevu nchini.
Dkt. Msuya aliongeza kwa kusema ruzuku hiyo ni sehemu ya juhudi za mfuko huo katika kuhimiza matumizi bora ya ardhi, uhifadhi wa mazingira na kuongeza pato la taifa kupitia kilimo cha kibiashara chenye tija.
“Tunatambua umuhimu wa kilimo cha miti ya mpira kama chanzo cha malighafi ya viwandani na mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kupitia ruzuku hii, tunalenga kusaidia NDC kufanikisha azma ya serikali ya uchumi wa kijani,” amesema.
TaFF ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, ambayo inasimamia uendelevu wa rasilimali za misitu nchini.
Dkt. Msuya amesema baadhi ya majukumu yao kama TaFF ni kufadhili na kuwezesha miradi ya uhifadhi wa misitu, kuhamasisha upandaji wa miti na kutoa elimu na uhamasishaji wa uhifadhi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Dkt. Yohana Mtoni, ameishukuru TaFF kwa kuunga mkono juhudi za shirika lake na kueleza ruzuku hiyo itatumika katika kuandaa vitalu, kupanda miche ya miti ya mpira, kutoa mafunzo kwa wakulima na kuweka miundombinu ya msingi katika maeneo ya mradi.
“Mradi huu utafungua fursa kwa vijana na wakulima wadogo kuingia kwenye kilimo cha miti ya mpira, ambacho kina faida za muda mrefu kiuchumi na kimazingira,” amesema.
Dkt. Mtoni ameongeza kwa kusema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mazingira yanayofaa kwa kilimo cha miti ya mpira, lakini alidai bado mchango wake katika sekta ya kilimo ni mdogo kutokana na changamoto ya rasilimali na uelewa mdogo miongoni mwa wakulima hivyo aliahidi kuwa ruzuku iliyotolewa itasaidia kuchochea mabadiliko chanya katika sekta hiyo.
Aidha amesema kilimo cha miti ya mpira si tu kwamba huongeza kipato kwa wakulima, bali pia husaidia kuhifadhi udongo, kurejesha uoto wa asili na kupunguza hewa ukaa, hivyo kuchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
NDC ni shirika la umma nchini Tanzania lililoanzishwa kwa lengo la kuendeleza shughuli za kiuchumi na kukuza uwekezaji katika sekta mbalimbali za kimkakati.
Baadhi ya majukumu ya msingi ya NDC ni pamoja na Kuchochea Maendeleo ya Viwanda, Kuhamasisha na Kuratibu Uwekezaji, Kusimamia Mali na Miradi ya Serikali na Kuendeleza Kilimo Biashara na Uzalishaji wa Malighafi.