NDC, Labio Farm Cuba zajadiliana uzalishaji bidhaa za kibaolojia 

Na Mwandishi Wetu, Pwani

SERIKALI ya Cuba kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, zimeanza rasmi mazungumzo ya kuona namna ya kuongeza bidhaa mbalimbali za kibaolojia ikiwemo uzalishaji wa mbolea hai kupitia katika Kiwanda cha Viuadudu cha TBPL kilichoko Kibaha mkoani hapa.

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole wakati akizungumzia majadiliano yanayoendelea hivi sasa baina ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) pamoja na Kampuni ya Labio Farm kutoka nchini Cuba ambayo yanafanyika jijini Dar es Salaam.

Balozi Polepole amesema miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika majadiliano hayo ni pamoja na uongezaji uzalishaji wa bidhaa mpya za kibaolojia pamoja na uhaulishaji wa teknolojia.

Amesema licha ya kiwanda hicho kwa hivi sasa kuzalisha dawa za viuadudu pamoja na viuatilifu hai mpango uliopo ni kuhakikisha uzalishaji wa mbolea hai pamoja na chanjo za wanyama zinafanyika kiwandani hapo.

Awali kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, viongozi wa Labio farm kutoka nchini Cuba walipata fursa ya kutembelea katika kiwanda hicho kilichoko Kibaha na kujionea namna uzalishaji wa bidhaa za kibaiolojia unavyofanyika kiwandani hapo.

Akizungumza katika ziara ya kutembelea kiwanda hicho, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, amesema ujio wa ugeni huo kutoka Cuba na kutembelea katika kiwanda hicho ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba na watahakikisha wanashirikiana na Cuba katika kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha bidhaa mbalimbali za kibaolojia.  

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe (wa pili kulia), akiwa na ujumbe kutoka Kampuni ya Labio Farm ya Cuba wakati ujumbe huo ulipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha Viuadudu cha TBPL kilichopo Kibaha, Pwani.

Licha ya kupongeza jitihada hizo za serikali katika kuunga mkono kiwanda hicho, Dkt. amesema mazungumzo hayo ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha nchi inajikita zaidi katika kukuza diplomasia ya uchumi.

Kwa upande wa Mwakilishi wa Labio Farm, Julio Gomes, ameanisha kuwa nchi hiyo iko tayari kuchangia katika swala zima la kuangamiza malaria kupitia uzalishaji mkubwa kwa bidhaa za kutokomeza ugonjwa huo ikiwa ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo.

Kiwanda cha TBPL kinamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kikiwa ni cha kipekee Barani Afrika na kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za bidhaa za kibaolojia kwa mwaka, vilevile kina uwezo wa kuzalisha viuatilifu vya kibaiolojia (Bio-pesticides), mbolea hai (Bio-fertilizer), virutubisho vya chakula (Food Supplements) na aina mbalimbali za chanjo za wanyama.

Tanzania na Cuba zina ushirikiano mkubwa katika sekta mbalimbali ambao ulioasisisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *