Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
MADAKTARI Bingwa wabobezi wa upasuaji ubongo na mishipa ya fahamu kutoka nchi 12 duaniani wameweka kambi ya siku tano katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Lengo la kambi hiyo ni kubadilishana ujuzi, maarifa na uzoefu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya MOI kukifanya kitovu cha umahiri katika elimu na mafunzo ya tiba barani Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Abel Makubi aliyasema hayo jana katika ufunguzi wa mafunzo hayo.
Alisema MOI imeandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Umoja wa Madaktari wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu Ulaya (EANS) kwa lengo la kubadilishana uzoefu, ujuzi na washiriki wa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yanaakisi dhamira ya taasisi yetu kujikita katika umahiri wa kutoa elimu, mafunzo ikiwa ni sehemu ya mipango yetu.
“Kwa kuandaa tukio hili, tunawekeza katika huduma bora za afya kwa Tanzania ya sasa na badaye,” alisema.
Kwa upandew wake, Mkurugenzi wa Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu MOI, Dkt. Limery Mchome, alisema mafunzo hayo yameanza jana hadi Novemba 24, 2023.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wataalam kutoka nchi za Austria, Norway, Sweden, USA, Urusi, India, Jamhuri ya Czech, Kenya, Malawi, Zambia, Uganda na Tanzania.
Lengo ni kubadilishana ujuzi, kuongeza ufanisi katika utoaji huduma bora za kibobevu katika matibabu ya upasuaji kupitia kwenye fuvu, matundu ya pua bila kufungua fuvu.
“Kuna kozi maalum ya matibabu ya stroke, kama mgonjwa atawahishwa hospitali ndani ya muda mfupi tangu apate stroke, anaweza kupata matibabu hayo bila kufungua fuvu.
“Katika kambi hii tuna mafunzo ya kufanya operation kwa kutumia darubini rahisi, itawawezesha madaktari waliopo hospitali zisizo na darubini maalum ya kufanyia upasuaji, kufanya upasuaji huo ukiwa na matokeo mazuri,” alisema Dkt. Lemery.