NBC yazindua kampeni’NBC Shambani’msimu wa nne kwa wakulima wa Korosho Mtwara

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imeatambulisha msimu wa nne wa kampeni yake ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ Kwa wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara hususani kwa wilaya za Tandahimba na Newala. Hatua ya benki hiyo mwendelezo wa jitihada zake zinazolenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa zao la korosho mkoani humo kupitia huduma mahususi na zenye upendeleo kwa wakulima wa zao hilo.

Hafla ya utambulisho wa kampeni hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki wilayani Tandahimba ikiongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Francis Mkuti, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Michael Mntenjele, huku ikihudhuriwa na wadau mbalimbali zao hilo mkoani Mtwara wakiwemo wakulima pamoja na viongozi waandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya NBC Bw Rayson Foya.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mkuti pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kutoa kipaumbele kwa wakulima nchini kupitia huduma zake, alisema ujio wa kampeni hiyo wilayani mwake ni  ukombozi muhimu kwa wakulima wa korosho wanaohitaji upendeleo maalum wa huduma za kifedha na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha dhamira ya benki hiyo inafanikiwa.

“Zaidi nimefurahi kusikia kupitia kampeni hii wakulima wanaweza kupata mikopo ya vitendea kazi muhimu kama vile matrekta na zana nyingine za kisasa za kilimo, pembejeo za kilimo na  mikopo ya malipo  ya  awali kwa wakulima. Niwapongeze zaidi NBC kwa kubuni aina hii ya zawadi kwasababu zinalenga kuchochea pia kasi ya uzalishaji wa zao hili kwa Zawadi hizi ni sehemu ya zana za kilimo’’ anasema.

Zaidi Mkuti ameonyesha kuguswa zaidi na uhusishwaji wa huduma za bima  za afya na kilimo  zinazotolewa na NBC kwenye kampeni hiyo kwa kuwa huduma hizo zina mchango muhimu zaidi kwa wakulima, hasa katika kukabiliana na changamoto za kiafya kwao binafsi  na familia zao na kujilinda dhidi ya hasara zitokanazo na majanga ya asili ambayo yamekuwa takiathiri mazao yao.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Foya anasema kampeni hiyo ni sehemu ya  mwitikio wa benki ya NBC katika kufanikisha mkakati wa serikali kupitia agenda ya 2010/30 inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030.

“Sambamba na uzinduzi wa kampeni hii kwa wakulima wa zao la korosho wilayani Tandahimba na Newala, pia tunatoa huduma mbali mbali kwao ikiwemo, ufunguaji wa akaunti za wakulima, ambazo hazina makato ya mwezi, huduma za mikopo kwa mkulima mmoja mmoja kwa ajili ya zana za kilimo kama matrekta na  mikopo kwa vyama vya ushrika (AMCOS/Union) kwa ajili ya pembejeo zao.’’ Anataja.

Foya anasema kupitia kampeni hiyo, benki ya NBC NBC inalenga kugusa sekta muhimu kitaifa kwa kuchochea ukuaji wa ajira kwa kuwa sekta hiyo inagusa ajira za watanzania kwa asilimia 65.

Wakifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Bw Raymond Urassa pamoja nae Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo, David Raymond wanasema inawalenga wakulima wote wakiwemo mmoja mmoja, vyama vikuu vya ushirika na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS)  ambavyo vitapitisha fedha za mauzo kwenye akaunti za NBC Shambani.

“Kupitia kampeni hii ambayo kwa mwaka huu tunaizindua kwa mara ya nne mkoani Mtwara  wakulima wa  korosho kwenye wilaya hizi mbili wataweza kujishindia vitendea kazi mbali mbali kama vile pampu ya kupulizia  dawa, baiskeli, pikipiki na maguta (pikipiki za miguu mitatu) huku vyama vikuu vya ushirika vikiwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi kuu ya kampeni hiyo ambayo ni trekta,” anasema Urassa.

Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wengine, Karimu Haji Swalehe na Sharifa Mohammed Nahunda waliishukuru na kuipongeza benki ya NBC kwa kampeni hiyo ambayo pamoja na kuwajengea uelewa zaidi kwenye masuala fedha, pamoja na kuwajengea utamaduni wa wao kujiwekea akiba pia walionyesha kuvutiwa na huduma za bima za afya na bima za kilimo kutokana na hitaji kubwa walilonalo wakulima hao kwenye masuala huduma bora za kiafya kwa ajili yao na familia.

Katibu Tawala (DAS) wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara, Francis Mkuti (alieketi) akijaribu ubora wa trekta ambalo litatolewa na benki ya NBC kama zawadi kuu kwa mshindi wa kampeni ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ inayoratibiwa na benki  hiyo mahususi kwa wakulima zao la korosho wilaya za Tandahimba na Newala mkoani Mtwara wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo ya miezi mitatu iliyofanyika jana wilayani Tandahimba mkoani Mtwara. Wanaoshuhudia ni pamoja na Ofisa Mkuu wa Fedha Benki ya NBC, Rayson Foya (aliepanda trekta kushoto), Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Mtwara, Robert Msunza (aliepanda trekta kulia), Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tandahimba na Newala (TANECU), Karimu Chipola (Katikati aliesimama) pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo na wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *