Waziri Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Saada Mkuya (katikati waliosimama) akiwashuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto -walioketi) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Yusuph Mwenda (Kulia – walioketi) wakitia Saini makubaliano yanayotoa fursa kwa benki hiyo kutumika kukusanya malipo mbalimbali ya Serikali ya SMZ kupitia mtandao na mfumo na wa kidijitali wa benki hiyo. Hafla ya utiaji Saini makubaliano hayo imefanyika hii leo Zanzibar ikiongozwa na Mkuya.(Picha:Mpigapicha Wetu)
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini hati ya Makubaliano (MOU) na taasisi sita za Serikali ya Mapinduzi Zanzbar (SMZ) yanayotoa fursa kwa benki hiyo kutumika kukusanya malipo mbalimbali ya serikali kupitia mtandao na mfumo na wa kidijitali wa benki hiyo.
Makubaliano hayo yanayohusisha Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mfuko wa Hifadhi Jamii Zanzibar (ZSSF), Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Idara ya Ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi- Zanzibar (ZPPP) na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yanatajwa kuwa mbali na kurahisiha huduma ya malipo kwa wananchi pia yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuzuia upotevu wa mapato ya serikali.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika leo Zanzibar ikiongozwa na Waziri Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Saada Mkuya huku ikihusisha uwapo wa viongozi waandamizi wa mashirika wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi.
Akizungumzia kwenye hafla hiyo, Mkuya pamoja na kuwapongeza wadau hao kwa ushirikiano huo amesema hatua hiyo inakwenda sambamba na adhima ya serikali ya SMZ kuelekea kukamilisha mfumo wake wa Serikali mtandao.
“Hatua hii ya leo kwa kiasi kikubwa inaunga mkono jitihada za serikali kutumia vizuri teknolojia na mifumo ya kielektroniki katika shughuli zake hususani katika ukusanyaji wa mapato. Hatua hii inatusaidia katika kurahisisha huduma za malipo mbalimbali kwa wananchi, kuongeza kasi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na zaidi pia kuzia mianya ya upotevu wa mapato ya serikali…tunawapongeza sana NBC na wadau wote kwa hatua hii,’’ amepongeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, amesema ushirikiano huo ni mwendelezo wa makubaliano ya awali ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonyesha dhamira thabiti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato yake kupitia mfumo wa Kielektroniki yaani (GEPG) au ZanMalipo.
“Kupitia makubaliano haya wananchi sasa wataweza kutumia mtandao wa Benki ya NBC kufanya malipo ya Serikali na ankara mbalimbali kupitia mtandao wa Benki ya NBC,’’ amesema.