Nala kitovu cha uwekezaji, fursa kubwa za viwanda na ajira nchini

Sarah Moses, Dodoma

MAMLAKA ya Uwekezaji Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeendelea kuimarisha juhudi za kuvutia wawekezaji katika eneo la Nala jijini Dodoma, likibuniwa mahsusi kuwa kitovu cha viwanda vya kimkakati na ajira nchini. 

Hatua hii inafuatia kutokana na uzinduzi rasmi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) uliofanyika Agosti 12, 2025.

Akizungumza leo Septemba 23,2025 jijini Dodoma Meneja wa Kanda ya Kati wa TISEZA, Venance Mashiba amesema eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 607 limeandaliwa kwa ajili ya kuendeleza viwanda vya kusindika mafuta ya kupikia, bidhaa za nyumbani, teknolojia, madawa na huduma nyingine za kijamii.

Amesema kuwa tayari wawekezaji wameanza kuitikia wito ambapo wanne wamejitokeza huku akitolea mfano Kiwanda cha Karibu Natural Limited chenye thamani ya dola milioni 4, ambacho kipo katika hatua za mwisho za kukamilika na kitakachoajiri zaidi ya wafanyakazi 100 wa moja kwa moja.

“Hii ni ishara kuwa Nala imekuwa kivutio halisi cha uwekezaji,tumeboresha mazingira kuanzia barabara, upatikanaji wa ardhi bila malipo, hadi vivutio vya kodi kwa watakaowekeza kuanzia mitaji ya dola milioni 5,tunataka Nala iwe kitovu cha viwanda vitakavyohudumia Dodoma na taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema kuwa hadi sasa maombi manne ya wawekezaji wa ndani yamepokelewa, huku mazungumzo yakiendelea na wawekezaji wa kimataifa. Lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, Nala linakuwa na zaidi ya viwanda 100 vitakavyoongeza ajira na mapato ya taifa.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TISEZA, Pendo Gondwe, amesisitiza kuwa mradi wa Nala ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya viwanda, na kwamba jamii inapaswa kufahamu kuwa eneo hilo lina miundombinu ya uhakika tayari kwa wawekezaji.

Hata hivyo naye Mwekezaji wa kiwanda cha Karibu Natural Limited, Varum Giyal, amesema kiwanda chake kitakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo hususan alizeti na mazao mengine ya mafuta yanayopatikana kwa wingi mkoani Dodoma na Kanda ya Kati.

“Lakini pia hii itaenda sambamba na kupunguza utegemezi wa mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi”amesema.

Amesema Nala imejipambanua kama kivutio kipya cha uwekezaji nchini Tanzania, chenye ardhi ya kutosha, mazingira rafiki ya biashara, vivutio vya kodi na mshirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *