KAIMU Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anaeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri, Dk. Eliza Mwakasangula amewakaribisha Watanzania wote kutembelea banda lao lililopo katika Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia katika viwanja hivyo amesema katika huduma mbalimbali ambazo zinatolewa katika chuo hicho hivyo wafike kuweza kujionea.
“Tunawakaribisha watu wote kwani tunahuduma mbalimbali, tunadahili wanafunzi kwaajili ya kujiunga na Program zetu Chuo Kikuu Mzumbe kwa ngazi ya Shahada za awali kwa wale waliomaliza kidato cha nne, kidato cha Sita na hata waliomaliza muda mrefu,” amesema.
Amesema Chuo Kikuu cha Mzumbe ni miongoni mwa vyuo vinavyotoa Mafunzo mbalimbali ikiwemo masomo ya Biashara, Utawala, Sheria, Uhasibu, Sayansi na Teknolojia ambapo wanateknolojia mbalimbali kwa vijana wao ambao wamekuwa wakizianzisha chuoni hapo.
“Chuo chetu kina kampasi tatu ambapo ni Mkoa wa Morogoro, Dar es Salaam maeneo ya Upanga na Tegeta pamoja na mkoani Mbeya,” amesema.
Aidha Dk. Eliza amewaomba Watanzania wakiwemo Wanafunzi waliomaliza Chuo hicho miaka ya nyuma (Alumni) kujitokeza na kuchangia kampeni ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike mkoani Mbeya.
Amesema kwa kufanya hivyo ni ishara ya
kurudisha kitu kidogo kwa jamii ikiwa nao ni wanajamii wa Chuo Kikuu Mzumbe.
“Ujenzi wa bweni hilo tayari umezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambapo kuna namba maalum ya uchangiaji hivyo niwakaribishe wanafunzi waliosoma Mzumbe kuweza kuchangia,” amesema.
Licha ya kuwakaribisha pia amewaomba wananchi kwa ujumla kuchangia ujenzi wa hosteli za Wanachuo wa kike katika kampasi ya Mbeya kupitia control namba 994180331310.