Na Badrudin Yahaya
LICHA ya kupokea ofa kutoka kwa timu za Kaizer Chiefs na Wydad Casablanca lakini mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize ameweka wazi dhamiri yake ni kutaka kuendelea kuitumikia timu yake.
Mzize amesema kuwa, anaziheshimu timu zote ambazo zimeonesha nia ya kumsajili lakini alidai bado
anataka kuendelea kujikuza zaidi ndani ya timu yake ya Yanga ambayo ndio iliyokuwa ya kwanza kumpa nafasi.
“Nimeona timu ambazo zinanihitaji zote ni kubwa na binafsi nilifarajika kwakuona kuwa kumbe kiwango
changu kinaonekana, hata hivyo kulingana na umri wangu bado nahitaji kuendelea kujifunza zaidi,” alisema.
Mzize alipandishwa katika kikosi cha Yanga SC msimu wa 2021-22 akiwa chini ya Kocha, Nasreddine Nabi
ambaye kwasasa anafundisha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Katika misimu ambayo amecheza ndani ya Yanga tayari amefanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi na FA lakini pia ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi msimu wa 2021-22 na msimu wa 2023-24 ameshinda Tuzo ya Mfungaji Bora wa michuano ya FA.
Licha ya uwepo wa washambuliaji kama Prince Dube na Jean Baleke lakini chini ya Kocha, Miguel Gamondi, Mzize ameendelea kuaminika na tayari ameshafanikiwa kufunga bao moja katika msimu mpya wa ligi ambapo Yanga wamecheza mechi moja.