Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Mohamed Besta (kushoto) akisaini mikataba ya ujenzi na wakandarasi walioshinda zabuni za ujenzi wa Miundombinu ya Usafiri Haraka wa Mabasi (BRT Phase 4), Jijini Dar es Salaam na ujenzi wa barabara ya TAMCO – Vikawe hadi Mapinga kwa kiwango cha lami; sehemu ya Pangani hadi Mapinga (Km 13.59).
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya pamoja na Viongozi wengine wakishuhudia zoezi hilo lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Mikataba 5 ya ujenzi wa miundombinu hiyo imesainiwa Jana
Mkataba wa kwanza uliosainiwa ni ujenzi wa Miundombinu ya barabara yenye urefu wa Km. 13.5 kuanzia Maktaba ya Taifa mpaka Mwenge ikijumuisha kipande cha Barabara ya Sam Nujoma kutoka Mwenge mpaka Ubungo. Mkataba huu pia unahusisha upanuzi wa Daraja la Selander, ujenzi wa Vituo Vikuu Viwili vya Mabasi, Vituo vya Kawaida vya Mabasi Ishirini (20) na Vituo Mlisho (Feeder Station) kumi (10) ambapo mkandarasi aliyeshinda ni Kampuni ya China Geo – Engineering Corporation kutoka China na ujenzi umepangwa kukamilika kwa muda wa miezi 18.
Mkataba wa pili ni ujenzi wa Miundombinu ya barabara yenye urefu wa Km 15.63 kuanzia Mwenge mpaka Tegeta. Mkataba huu pia unahusisha upanuzi wa Madaraja matatu, (Mlalakuwa, Kawe na Tegeta), ujenzi wa Vituo Vikuu vya Mabasi, Vituo vya Kawaida vya Mabasi Kumi na Tisa (19) na Vituo Mlisho (feeder station) Vitano (5) ambapo mkandarasi aliyeshinda ni Kampuni ya Shandong Luqiao Group Co., Ltd kutoka China na ujenzi umepangwa kukamilika kwa muda wa miezi 18.
Mkataba wa tatu ni ujenzi wa Karakana (Depot) Mbili na Kituo Kikuu cha mabasi kimoja ambapo mkandarasi aliyeshinda ni Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd kutoka China na ujenzi umepangwa kukamilika kwa muda wa miezi 18.
Mkataba wa nne unahusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara na upanuzi wa sehemu ya barabara ya Ubungo hadi Kimara yenye urefu wa Km 5 kutoka njia 6 hadi njia 8 kwa lengo la kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara ambapo mkandarasi aliyeshinda ni Kampuni ya Sichuan Road & Bridge (Group) Corporation Ltd kutoka China na ujenzi umepangwa kukamilika kwa muda wa miezi 18.
Mkataba wa tano unahusu ujenzi wa barabara ya TAMCO – Vikawe hadi Mapinga kwa kiwango cha lami; sehemu ya Pangani hadi Mapinga (Km 13.59) ambapo mkandarasi aliyeshinda tuzo ni Kampuni ya Kings Builders Ltd.