Na Daniel Mbega
TAKRIBAN miaka 20 iliyopita nilikuwa miongoni mwa wahanga wa kugombea daladala na hata kupitia madirishani kama ilivyokuwa ada kwa wakazi wa maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam, hususan Mbagala na Gongo la Mboto.
Shida ya usafiri ni miongoni mwa kero ambazo zinawatesa wakazi wa jiji hilo, ambalo licha ya idadi ya watu kupungua kutokana na wakazi wengi kuhamia Dodoma baada ya Serikali kuhamishia makao yake makuu huko, lakini bado changamoto ni kubwa.
Katika kipindi kile haikuwa ajabu kumuona mwanamke akipambana kupitia dirishani, maana kinyume chake ‘angeweza kukesha’ kituoni akisubiri daladala lenye nafasi – ambalo ni adimu hata hivyo.
Siyo kwamba shida ile imepungua. La hasha. Bado ingalipo na kwa sasa wakazi wa Kusini mwa Dar es Salaam wanaotumia Barabara ya Kilwa pamoja na wale wa Gongo la Mboto ambao wanatumia Barabara ya Nyerere wanalazimika kuingia gharama mara mbili ili waweze kupata usafiri wanapokwenda kazini asubuhi na wanaporejea majumbani jioni.
Ndiyo. Kwa mfano, wakazi wa Mbagala, Kongowe, Mbande na maeneo mengine ya Kusini mwa Dar, ili waweze walau kupata nafasi kwenye daladala wanalazimika kutembea hadi Bandari (Bendera Tatu) kutoka Shule ya Uhuru au Stesheni, ambako wanalipa nauli ya kugeuza na ile ya kuwapeleka majumbani kwao – nauli mara mbili!
Ni adha iliyoje, hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi umebana na bei ya bidhaa iko juu.
Adha hii ilikuwa ikiwapata pia wakazi wanaotumia Barabara ya Morogoro (Ubungo, Kimara na Mbezi), lakini kwa sasa walau mambo yamekuwa nafuu kwao kutokana na uwepo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) pamoja na kupanuliwa kwa barabara, hivyo kupunguza msongamano.
Msongamano katika Barabara ya Nyerere siyo mkubwa sana baada ya kukamilika kwa Daraja la Mfugale pale Tazara, lakini hii hawaondolei adha ya usafiri wakazi a Gongo la Mboto, Pugu na Chanika, maeneo ambayo – kama ilivyo kwa Mbagala – yana idadi kubwa ya wakazi kwa sasa kulinganisha na miaka iliyopita.
Msongamano huu wa magari bado ungalipo katika barabara hizo kuu mbili, lakini kuna kila dalili kwamba utakuwa historia baada ya muda mfupi. Kwa sasa msongamano huo umeongezeka kutokana na ujenzi wa barabara za mwendokasi unaoendelea.
Na kwa kadiri ya mambo, kukamilika kwa barabara za mwendokasi na ujio wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka, kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Serikali ya Awamu ya Sita imeona adha hizi na ndiyo maana hivi sasa Rais Samia Suluhu Hassan mwendokasi wake unatisha. Anataka kuhakikisha kero ya msongamano wa magari inakwisha kwa kujenga barabara za mwendokasi kila mahali.
Ukiacha awamu ya pili ya ujenzi wa mradi wa Mwendokasi unaoendelea katika Barabara ya Kilwa, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa Mwendokasi kwa ujenzi wa Barabara ya Nyerere (Gerezani – Gongo la Mboto) kuhakikisha kwamba mabasi ya mwendokasi yanafika kila kona na kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri.
Ujenzi huo unaendelea kwa kasi ya ajabu hivi sasa na kama kasi hiyo itaendelea, mradi huo utakamilika kwa wakati.
Kasi ya Rais Samia ilianza Desemba 4, 2021, wakati alipoweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka Awamu ya Pili katika barabara za Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa jijini Dar es Salaam, hafla ambayo ilifanyika katika Karakana Kuu ya Mradi huo, Mbagala Rangitatu jijini humo.
Mradi huo unasimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) na unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa Shs. 327.351 bilioni na fedha za serikali Shs. 40.679 bilioni.
Serikali ilipanga kwamba barabara hii ya Mwendokasi kutoka Gerezani – Mbagala na michepuo yake yenye urefu wa jumla ya kilometa 20.3 ikamilike Aprili 2023 ikiwa na vituo 17 na barabara za juu tatu.
Hata hivyo, kutokana na changamoto kadhaa, mradi huo bado haujakamilika ingawa uko katika hatua za mwisho.
Wananchi walionja raha ya usafiri wa mwendokasi mwezi Julai wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (Saba Saba) baada ya Serikali kuamua kutumia kwa muda usafiri huo kutoka Gerezani hadi Mbagala.
Katika kipindi hicho, msongamano ulipungua kwa kiasi cha kutosha, na wengi walikuwa wanaombea usafiri huo ungeendelea hata baada ya maonyesho hayo, lakini kwa vile bado kuna hatua za kukamilisha, itabidi waendelee kusubiri kwa muda.
Mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara ya mwendokasi kutoka JKT Mgulani kupitia Kigogo hadi Magomeni katika Barabara ya Kawawa kuungana na ile inayokwenda Morocco.
Katika mtandao huo wa Mabasi Yaendayo Haraka kutakuwa na barabara mpya kutoka Tabata Segerea hadi mzunguko wa Kigogo katika Barabara ya Kawawa.
Kadhalika utafanyika upanuzi kutoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Vikindu katika Barabara ya Kilwa.
Kwa awamu zote sita zitakapokamilika kutakuwa na kilomita 154.6.
Kwa sasa mwendokasi wa Mama Samia unaendelea katika barabara inayoanzia Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto yenye urefu wa kilomita 23.6, ambapo ujenzi wake utagharimu Sh231 bilioni.
Mradi huo utakaoanzia katika barabara ya Azikiwe karibu na kituo cha mwendokasi cha Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto, utajumuisha tawi la kutokea Daraja la Mfugale katika barabara ya Mandela hadi Buguruni, kupitia barabara ya Uhuru hadi Gerezani kupitia barabaraa za Shaurimoyo na Lindi.
Mradi huo utachukua muda wa miezi 36 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2025.
Mama Samia haishii Gongo la Mboto, kwani kasi yake itaendelea katika Awamu ya Nne ambapo ujenzi utahusisha barabara za Bagamoyo hadi Tegeta, Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma zenye urefu wa kilometa 25.9 na awamu ya tano itahusisha ujenzi wa barabara za Mandela kuanzia eneo la Ubungo kupitia Tazara, Uhasibu kuungana na barabara ya Kigamboni na barabara ya kuanzia Tabata Relini hadi Segerea.
Itakumbukwa kuwa, taasisi maalumu ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambayo iko chini ya Tamisemi, ilianza ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza Agosti 2010 ukiwa wa kilomita 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni.
Awamu hiyo ni pamoja na kutoka Magomeni – Barabara ya Kawawa hadi Morocco.
Pia kutoka Kituo Kikuu cha Zimamoto (Fire), Barabara ya Msimbazi hadi Gerezani, Kariakoo mbapo Mradi wa Awamu ya Kwanza ulikabidhiwa kwa serikali Februari 2016 na kuanza kazi Mei 16, mwaka huo ukigharimu jumla ya Shs. 385 bilioni.
Kwa hakika, kasi hii ya Rais Samia haipimiki na inalenga kuharakisha maendeleo na hivyo kukuza uchumi.