Na Badrudin Yahaya
Klabu ya Bayern Munich ambao ni mabingwa wa Ujerumani, wamefikia makubaliano ya kumsajili Mtanzania, Nestory Irankunda kutoka Klabu ya Adelaide United inayoshiriki Ligi ya Australia.
Usajili huo utakamilika kipindi cha majira ya kiangazi (Juni) ambapo Bayern watalipa ada ya pauni milioni 3 ili kunasa saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 17.
Irankunda ana uraia wa Tanzania akiwa amezaliwa katika Mkoa wa Kigoma lakini kwasasa ana miliki pasipoti ya nchini Australia na hivyo anaweza kuliwakilisha taifa hilo pia kimichezo.
Ameshacheza mechi kadhaa kwenye hatua za vijana lakini bado hajatumika katika timu ya taifa ya wakubwa na hivyo nafasi ya yeye kuitumikia Tanzania bado ipo.
Wazazi wa Irankunda ni raia wa Burundi lakini walihamia Tanzania na kujiunga na kambi za wakimbizi mkoani Kigoma na baadaye Irankunda akazaliwa akiwa hapa nchini Tanzania.