Na Mwandishi Wetu, Ifakara
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya sh milioni 900 kwa Halmashauri ya Ifakara Mji.
Akizungumza Novemba 6, 2023 mjini hapa, Mbunge wa Kilombero Abubakar Asenga, alisema ujio wa vifaa hivyo utasaidia kuboresha huduma za afya hivyo wanaishukuru serikali kwa hatua kubwa ya maboresho katika sekta hiyo.
Alieleza kuwa, jimbo hilo lilikuwa na kero saba muhimu na kubwa ambazo hazijawahi kutatuliwa tangu kupata Uhuru lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitatua ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara, maji, ukarabati kituo cha umeme Kidatu, ujenzi wa shule za kata, vituo vya afya, zahanati na hospitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, alisema ujio wa vifaa tiba hivyo ni neema kwa halmashauri hiyo.
Alisema, maboresho hayo makubwa yanayofanywa na Rais Samia ni lazima kuungwa mkono na watendaji hivyo akatoa siku 15 kuhakikisha MSD inafunga vifaa hivyo na wananchi wanaanza kupata huduma.
“Nawaomba MSD walete wataalamu wao kwa ajili ya kufunga vifaa hivi, haiwezekani Rais wetu afanye mambo makubwa kama haya watendaji tumuangushe, ni muhimu kuhakikisha tunasimamia na wananchi wanaanza kupata huduma kwa wakati,” alisema.
Naye Mwakilishi wa MSD ambaye ni Mfamasia na Afisa Huduma kwa Wateja Kanda ya Dar es Salaam, Diana Kimario, alisema kanda hiyo inahudumia mikoa mitatu ambayo ni Pwani, Morogoro na Zanzibar ambapo Ifakara ni mnufaika.
“Ujio wa vifaa hivyo vyenye thamani ya Shs. milioni 900 ni muendelezo wa mabadiliko makubwa katika maboresho sekta ya afya, sisi watumishi ndani ya MSD tunajivunia namna serikali yetu chini ya Rais Dkt. Samia na Mkurugenzi wa Bohari Mavere Tukai wanavyohakikisha tunafanya kazi bila hofu,” alisema.