Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, ameuhakikishia uongozi wa Bohari ya Dawa (MSD) kuwakabidhi eneo la ujenzi wa ghala la kuhifadhia bidhaa za dawa mkoani humo kabla ya Januari, 2024 ili kurahisisha usambazaji dawa.
Mongella alisema hayo katika kikao kazi cha MSD na wateja wake Kanda ya Kilimanjaro kilichofanyika mkoani Arusha na kuipongeza bohari hiyo kwa kusambaza bidhaa za dawa nchi nzima mbali ya uwepo wa changamoto za miundombinu kwa baadhi ya maeneo.
“Niahidi kwa Mkoa wa Arusha, mwenzangu wa Manyara kiwanja walishakabidhi, Mkoa hadi tunafika mwaka mpya tutakuwa tumekabidhi kiwanja.
“Nashauri tuweke mifumo imara ya kidigitali ambayo itasaidia sana kuimarisha mnyororo wetu wa thamani ili kuondoa changamoto nyingi zilizopo,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa usiku na mchana kuimarisha sekta ya afya ambayo ni sekta ya msingi kwa Watanzania.
Aliwashauri wasimamizi taasisi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia ili kuhakikisha Taifa linapiga hatua kubwa ya maendeleo.
“Niseme tu kwamba, Serikali ya awamu ya sita Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia tumeona kazi kubwa ambayo inafanyika kwenye sekta ya afya.
“Mkurugenzi Mkuu wa MSD ameonesha kwamba hata viwango vya ufanyaji kazi vimevunja rekodi za nyakati zote kwenye nchi yetu,” aliongeza Mongella.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema Bohari ya Dawa imedhamiria kupunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji bidhaa za dawa kutoka nje, kuongeza uzalishaji nchini, kupunguza uagizaji bidhaa.
“Tulikuta taasisi ina asilimia 34 tu ya bidhaa muhimu ambazo zina mikataba ya muda mrefu lakini kwa sasa tumeshavuka asilimia 90.
“Katika upande wa miradi maalum ya ujenzi wa vituo vipya, mtaona kuna mabadiliko kwa sababu tumebadili mfumo mzima wa ununuzi.
“Naomba niseme kuwa, MSD ni taasisi iliyokomaa, mkiangalia ukuaji wa sekta ya afya miaka 10 iliyopita, kwa idadi ya watu tumeongezeka kwa asilimia 37, idadi ya vituo tumetoka 5,000 hadi 7,000, bado tunaendelea nadhani tutafika 8,000 Julai, 2024,” alisema.
Tukai alisema upande wa utunzaji bidhaa za dawa umeongezeka kwa kukodisha maghala tayari Bohari imeanza ujenzi kwa kuhakikisha Kanda zote zinakuwa na maghala ambayo yatatumika kutunza bidhaa za dawa.
“Kwa sasa asilimia 70 ya kanda zetu haziwezi kutunza mzigo wa zaidi ya miezi miwili, sera ya nchi inasema uwe na miezi mitano mpaka tisa.
“Tunapambana kujenga maghala ili kuhakikisha tunakuwa na viwango vya kimataifa katika kutunza bidhaa,” alisisitiza Tukai.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Damas Kayera, alisema mbali na changamoto zilizopo, MSD inaendelea kupiga hatua kwa kuhakikisha bidhaa za dawa zinafika kwa wakati ambapo kwa sasa usambazaji unafanyika kila baada ya miezi miwili.
“Kwa sasa bidhaa za afya zinafanyika kila baada ya miezi miwili hivyo hakuna kusubiri sana, tunaishukuru Serikali ya Tanzania, fedha za kununulia dawa, vifaa tiba na huduma za afya zimeongezeka,” alisema.