MSD kugawa vyandarua 709,118 shule zote Dar

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

MKOA wa Dar es Salaam umezindua rasmi programu ya kukagawa vyandarua zaidi ya 700,000 katika shule zote za msingi ambapo ugawaji vyandarua hivyo utafanywa na Bohari ya Dawa (MSD), Kanda ya Dar es Salaam kuanzisha leo.

Uzinduzi wa program hiyo umefanyika Dar es Salam jana, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila, kushuhudiwa na wadau mbalimbali.

Wadau hao ni pamoja na wataalam kutoka sekta ya afya ngazi ya Wilaya na Mkoa ambapo Chalamila aliitaka sekta ya afya mkoani humo kupuliza dawa ya kuua mbu katika maeneo yote ya jiji hilo ili kukabiliana na malaria.

Chalamila alisema Taifa lolote linalojiandaa kukua kiuchumi hujidhatiti lisipate madhara katika rasilimali watu ambapo leo Tanzania inazungumzia malaria lakini historia inaonesha nchi kama Marekani mgonjwa wa mwisho kuumwa malaria ilikuwa mwaka 1950.

“Hapa kwetu Tanzania Bara na Zanzibar, tumeshapishana sana katika udhibiti wa malaria, Zanzibar wamejitahidi kudhibiti malaria, natoa wito kwa wataaam wote wa sekta ya afya, wadau, waendelee na dhamira ya kugawa vyandarua na kuongeza kasi ya kudhibiti mbu kabla ya kufikia hatua ya kupevuka.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuita wawekezaji kuja kuwekeza na miongoni mwa wawekezaji hao tunao wenzetu kutoka Cuba ambao wamewekeza kaika kiwanda cha kutengeneza dawa ya viua dudu.

“Tunaweza kununua, kupuliza maeneo yote na sasa hivi tuna programu ya kuipendezesha Dar es Salaam na tunaelezwa hadi kufika mwaka 2025, jiji hili litakuwa moja ya Majiji makubwa saba Afrika,” alisema.

Aliongeza kuwa, haiwezekani jiji hilo likawekwa katika orodha ya majiji saba makubwa Afrika lakini watu wake wanaugua na kufariki dunia kwa sababu ya malaria.

Aliwaomba watalaam wa afya kuisaidia serikali ili kuhakikisha Dar es Salaam na Tanzania bila malaria inawezekana.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Rashid Mfaume, alisema ugonjwa wa malaria bado ni tatizo nchini, hata maeneo ambayo wanaona ni ya maambukizi yako chini ya asilimia 3.5 lakini kuna baadhi ya maeneo hali ya maambukizi iko juu.

“Upande wa Dar es Salaam tumeona maeneo ya Luhanga na Tungi Songani maambukizi yako juu, wajibu wetu lazima tujue malaria bado ni tatizo lakini kuna maeneo ambayo ni kero kubwa.

“Hakuna mdudu anayeishi muda mfupi kama mbu mpevu ambaye haishi zaidi ya wiki mbili lakini ukimsubiria apevuke hasa wa kike anaweza kutaga mayai 100 hadi 200, suala la kugawa vyandarua ni afua mojawapo lakini tunahamasisha afua nyingine za kupambana na malaria kama kusafisha mazingira,” aliongeza.

Alitoa maelekezo kwa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kupuliza dawa katika mazalia ya mbu, lengo ni kupambana na mbu hatua za awali kabla hajapevuka.

Dkt. Mfaume alisema ipo haja wakati wa kuandaa bajeti ya fedha kwa ajili ya kupambana na malaria kwa kutokomeza mbu, viongozi wa dini wasaidie kuhamasisha utumiaji vyandarua katika kaya hasa kwa watoto ambao ndio walengwa wa vyandarua hivyo.

Awali Frank Mpembeni ambaye alimwakilisha Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam, alisema usambazaji vyandarua katika Mkoa huo utafanyika katika wilaya zote tano.

Wilaya hizo ni Ubungo, Kigamboni, Temeke, Kinondoni na Ilala na kufafanua kuwa, kazi ya MSD katika program hiyo ni kupokea vyandarua, kutunza na kusambaza.

“Ubungo tutagawa vyandarua 122,116 katika shule 194, Kigamboni 44,311 katika shule 77 , Temeke 180,843 katika shule 152, Kinondoni 106,123 katika shule 175 Ilala 255,725 katika shule 280 hivyo kufanya jumla ya vyandarua vitakavyogawiwa kufikia 709,118.

“Katika usambazaji huu, tutatumia magari makubwa ya kuanzia tani tano, 10 na 15, pia tutatumia magari madogo kwenye maeneo ambayo magari makubwa hayawezi kufika kwa urahisi.

“Tunatarajia kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi wakuu wa shule,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *