Na Badrudin Yahaya
KLABU ya Simba, imekamilisha dili la kumsaini winga wa AS Vita, Elia Mpanzu kwa ada ya usajili inayotajwa kuwa ni dola 250,000 ambazo ni zaidi ya shilingi 682,500,000.
Mchezaji huyo ambaye alikuwepo kwenye dimba la Benjamini Mkapa kushuhudia mchezo kati ya Simba na Al Ahly Tripol uliopigwa Jumapili, anadaiwa kuwa amesaini mkataba wa miaka miwili na anatarajia kuanza kuitumikia timu hiyo kwenye michuano ya Shirikisho Afrika kwenye hatua ya makundi.
Hata hivyo Mpanzu atalazimika kusubiri hadi Desemba 15, mwaka huu wakati dirisha dogo la usajili litakapofunguiliwa ili jina lake kuingizwa rasmi kwa ajili ya kuanza kutumika kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara na CRDB Bank Federation Cup.
Simba imekuwa wakimfuatilia Mpanzu kwa muda mrefu lakini usajili wake ulikwama kwenye dirisha kubwa la usajili baada ya mchezaji huyo kupata dili la kwenda kufanya majaribio nchini Ubelgiji katika timu ya KRC Genk.
Kutokana na kushindwa kufaulu kwenye majaribio hayo, Simba ilirudi tena na ofa yao mezani na kiongozi katika mazungumzo hayo anatajwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Muhene ‘Try Again”.
Simba inajaribu kuimarisha safu yao ya ushambuliaji hasa katika maeneo ya pembeni ambapo kwasasa kuna Joshua Mutale, Edwin Balua, Kibu Denis, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka.
Wakati huo huo, taarifa kutoka ndani ya Simba, zinadai nafasi ya Kipa, Ayoub Lakred ndani ya timu hiyo imezidi kuwa finyu baada ya ujio wa Mpanzu.
Kipa huyo aliumia wakati wa maandalizi ya msimu ambapo iliwafanya Simba kutafuta kipa mwengine, Moussa Camara ambaye kwasasa anafanya vizuri kwenye milingoti mitatu.