Na Mwandishi Wetu, Dar es Saslaam
SERIKALI imeshakamilisha mpango wa miaka 10 wa mkakati wa mfumo wa uchumi wa kidijitali wa kitaifa (DEF) kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2033 sambamba na kuboresha matumizi ya teknolojia ya kidigitali katika huduma za serikali na sekta binafsi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ambaye pia Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Mapinduzi ya Kidigitali cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Bw Mohammed Khatibu Abdulla, amesema wizara yake ilishakamilisha mpango huo na kinachosubiriwa kwa sasa idhini ya utekelezaji wake.
“Mpango wa mkakati wa mfumo huo (DEF) ilibuniwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa kibinafsi na umma kupitia vikao vya kiufundi vilivyoratibiwa na wizara yetu,” alisema Abdalla kwenye kikao Maalum cha Kikundi Kazi cha Mapinduzi ya Kidijitali jijini Dar es Salaam jana.
Abdulla alisema ujenzi wa misingi imara ya kidigitali hapa nchini yenye uwiano sawia, serikali imefanya kazi kwa pamoja na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za sekta binafsi, vyuo vikuu, makundi mbalimbali ya kijamii na washirika wa maendeleo.
“Kwa jitihada hizi za ushirikiano, Tanzania imefanya maendeleo makubwa katika kuunda mazingira muhimu kufikia maono yetu kama nchi. Takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa lam usajili laini za simu kutoka milioni 55.7 Aprili 2022 hadi milioni 62.3 kufikia Aprili 2023,” alisema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, watumiaji wa mtandao wa intaneti pia waliongezeka kutoka milioni 29.9 hadi miliono 33.1 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.1.
Abdulla alibainisha kuwa idadi ya watumiaji wa huduma za pesa kupitia simu za mkononi imeongezeka kwa asilimia 24.1 kutoka milioni 35.7 hadi milioni 44.3 na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali.
“Serikali kupitia wizara yangu imeshakamilisha pia Sera ya Taifa ya Tehama 2023, Sera ya Taifa ya Ubunifu 2024, Mpango wa Miundombino ya Umma ya Tanzania 2023/24, Mwongozo wa Usanifu wa Taasisi ya Tanzania 2024, Mkakati wa Digitali wa Tanzania na Mwongozo wa Ubadilishanaji wa taarifa na uuganishaji wa mifumo ya Tehama na Sheria ya Tehama ya Kitaifa,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga alisema Baraza ndiyo chombo cha juu cha majadiliano (PPD) hapa nchini na wajumbe wake ni viongozi wote kwa kitaifa, mawaziri wote pamoja na viongozi wote wa sekta binafsi.
“Kikundi kazi cha Mapinduzi ya Kidijitali kitatoa mchango mkubwa na hasa kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta nyingine za maendeleo na uchumi. Kikosi kazi cha Mapinduzi ya Kidigitali ni matokea ya Mkutano wa 14 wa TNBC,” alisema Dkt Wanga.
Alisema, mikutano yote ya TNBC inaongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye huongoza majadiliano hayo ya hatua ya juu yanayojumuuisha sekta za umma na binafsi.