ROMA, Italia
KOCHA wa AS Roma, Jose Mourinho, amefungiwa mechi mbili baada ya kukwaruzana na mwamuzi wa akiba wakati timu yake ilipofungwa mabao 2-1 na Cremonese Jumanne katika Serie A.
Mourinho alioneshwa kadi nyekundu kwa mara ya tatu msimu huu ikiwa zimepita dakika mbili tangu kuanza kwa kipindi cha pili baada ya kutupiana maneno na mwamuzi huyo.
Bao la Leonardo Spinazzola, lilifuta bao la kutangulia lililofungwa na Frank Tsadjout kwa mwenyeji, lakini Mourinho akiwa jukwaani alishuhudia Daniel Ciofani akifunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti ikiwa ni ushindi wao wa kwanza msimu huu na pia ni wa kwanza ikipita miaka 26 ndani ya Serie A.
Mourinho aliendelea kuzozana na waamuzi hao hata walipokuwa katika vyumba vya vya kubadilishia nguo baada ya mchezo huo kumalizika na sasa atakosekana katika mechi mbili pamoja na faini ya dola 10,000.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Serie A, ilieleza kwamba kocha huyo amefungiwa kutokana na kupinga uamuzi wa mwamuzi kwa nguvu na uchochezi katika dakika ya pili ya kipindi cha pili na kurudia tabia hiyo wakati wa kutolewa nje kwa kadi nyekundu”.