Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), jana imesaini mkataba wa makubaliano na Kiwanda cha Kairuki KPTL ili kuboresha upatikanaji wa dawa katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga na Mloganzila.
Mkataba huo umeanisha maeneo mawili, kuboresha upatikanaji wa dawa zisizopatikana kirahisi katika soko.
Dawa hizo ni pamoja na zile zinazotumika katika upandikizaji viungo mbalimbali mwilini kama figo, kongosho na dawa zenye ujazo mdogo ambazo zinatumika kwa watoto, wagonjwa wa saratani.
Eneo la pili la makubaliano ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Muhimbili katika uzalishaji dawa, namna ya kuzitumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, amesema hiyo ni hatua nzuri kuwepo kwa kiwanda cha dawa kinachomilikiwa na wazawa, kukidhi viwango vinavyohitajika.
Alisema Muhimbili ni Hospitali ya Rufaa ya kitaifa ambayo ni kubwa kuliko zote nchini yenye vitanda 2,150 ambapo upanga kuna vitanda 1,550, Mloganzila vitanda takribani 600 hivyo inahudumia watu wengi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Dkt. Muganyizi Kairuki, alisema kiwanda kimedhamiria kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji yaliyopo na kuhakikisha mkataba uliopo unakuwa na tija kwa hospitali.