Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inatarajia kufanya kambi maalum ya upasuaji wa kuweka nyonga na magoti bandia kwa wagonjwa wenye changamoto za maradhi ya nyonga na magoti.
Kambi hiyo itafanywa kwa kushirikiana na Hospitali ya Queen Elizabeth ya nchini Uingereza kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 1, 2023.
Akizungumzia kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji Mifupa, Nyonga na Magoti, Dkt. Shilekirwa Makira alisema wagonjwa watakaonufaika na huduma hizo ni wenye matatizo ya nyonga zilizosagika zenye maumivu makali na magoti yaliyosagika.
Dkt. Makira aliongeza kuwa watu wenye changamoto hizo watabadilishiwa kwa kuwekewa nyonga na magoti bandia kitu kitakachowafanya waondokane na maumivu wanayoyapata kabla ya nyonga zao kubadilishwa.
“Tungependa watu wajitokeze na kujisajili mapema kabla ya tarehe 27.11.2023 ili hospitali iweze kufanya maandalizi stahiki ikiwemo pamoja na kufanya vipimo vya awali ambayo ni muhimu kabla ya kufanya upasuaji huu,”alisisitiza Dkt. Makira.
Dkt. Makira aliongeza kuwa waliojiunga na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya, mfuko unagharimia zaidi ya asilimia 90.
Alisema bima zingine zinagharimia matibabu hayo hivyo wasisite kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo adhimu.
Aidha, alisema endapo kutakua na ushauri au kuweka miyadi (appointment) unashauriwa kuwasiliana na Madaktari Bingwa Idara ya Magonjwa ya Mifupa na ajali ambao ni Dkt. Makira simu namba 0765958302, Dkt. Abuu 0715219175 na Dkt. Amos 0683680522.