Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Soka ya Mlandege ya visiwani Zanzibar, imetetea taji lao la Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Simba SC bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa New Amani Complex.
Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Mlandege kupata ushindi ndani ya dakika 90 baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mechi zao tano za michuano hii mwaka huu.
Shujaa wa Mlandege katika mchezo alikuwa ni mshambuliaji, Joseph Akandwanao ambaye alifunga bao la ushindi dakika ya 54 ya mchezo.
Akandwanao pia alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo wa fainali na alizawadiwa shilingi milioni 2 kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC)
Simba licha ya kumiliki mpira kwa asilimia kubwa lakini ilikuwa ngumu kwao kupenya ukuta wa Mlandege ambao muda mwingi walicheza kwa kujilinda.
Huo unakuwa ni ubingwa wa pili mfululizo kwa Mlandege ambao msimu uliopita pia walishinda taji hilo kwa kuifunga Singida FC 2-0 kwenye mchezo wa fainali.
Simba ambao wameshinda taji hilo mara nne, walikuwa wanasaka taji lao la tano ili kuwafikia vinara Azam ambao wanaongoza kwa kushinda taji hilo mara nyingi zaidi.
Huu ni mchezo wa sita wa fainali wa michuano ya Mapinduzi Cup kwa Simba kupoteza na kuweka rekodi kuwa timu iliyopoteza fainali nyingi zaidi
Mshambuliaji wa Singida FG, Mkenya, Elvis Rupia amefanikiwa kuwa Mfungaji Bora wa michuano hiyo akiwa na mabao matano.