Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kuona ushiriki mkubwa zaidi wa Makandarasi wazawa katika kazi za utekelezaji wa ujenzi wa miradi nchini.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, aliyasema hayo jana katika mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, Makandarasi na Washauri elekezi wa ndani jijijini Dodoma, kujadili nafasi yao katika utekelezaji wa miradi.
Alisema Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kutenga miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa ajili ya makandarasi wa ndani ili waweze kukua na kupata uzoefu.
“Mwaka wa fedha 2023/204, miradi minne ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 kila mmoja, imetengwa kwa Makandarasi wa ndani tu.
“Kwa hiyo kilometa 200 zitajengwa na wazawa, hii ni fursa kubwa ya kuwasaidia,” alisema Bashungwa.
Alisisitiza kuwa, mwaka wa fedha 2023/2024 kilometa 20 za barabara zimetengwa kwa Makandarasi wanawake, zitagawanywa katika vipande vya kilometa tano tano.
Kazi hizo zitashindanishwa kwa kampuni za wanawake peke yao, hii inafanya jumla ya km 220 kujengwa na Makandarasi wazawa mwaka 2023/24.
Bashungwa alisema kazi za matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zenye thamani ya sh. bilioni 600 zitatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu katika mikoa yote 26 nchini.
“Mwaka wa fedha 2023/2024 kazi zote za matengenezo ya barabara kwa mikoa yote 26 nchini, Rais Dkt. Samia ameamua zitekelezwe na Makadarasi wa ndani”, alisema.
Alifafanua kuwa, Sheria ya Ununuzi wa Umma imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mradi ambao utatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu bila kushindanishwa na Makandarasi wa nje.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Makandarasi kuchangamkia fursa ambayo Rais Dkt. Samia ametoa kwa Makandarasi wa ndani, kuacha kudharauliana ili kupata maendeleo kwao na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Nchemba alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuongeza fedha kila mwezi kwa Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ili iweze kuongeza kasi ya kulipa madeni ya Makandarasi wazawa.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, alisema Ilani ya CCM imeahidi kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa Makandarasi wa ndani na kuwasisitiza kufanya kazi kulingana na miiko ya taaluma yao.
Dhima kuu ya mkutano huo ni kujadili, kudadavua mikakati mbalimbali kati ya Serikali na wadau wa sekta ya ujenzi kuhusu kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa na Washauri elekezi.