Na Jabir Johnson, Kilimanjaro
MOSHI ni miongoni mwa miji mikongwe nchini Tanzania. Historia inaonyesha kwamba ulianzishwa hata kabla ya Jiji la Arusha na Nairobi na ndiyo sehemu ambayo Serikali ya Wajerumani ilifanya kuwa Kambi ya Kijeshi mnamo mwaka 1892.
Mnamo mwaka 1926 mMji wa Moshi ulipewa hadhi ya kuwa mji mdogo, ambapo mchakato wa kwenda mji mdogo ulianza mnamo mwaka 1923. Ilipofika mwaka 1956 Moshi iukapewa hadi ya kuwa Mji kamili.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mkuu wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Tanzania (TRITA) kilichopo mjini Moshi, SP Ignatius Mganga, anasema Mji wa Moshi ulianzishwa na wahamiaji wa Kijerumani.
Aidha, Mji wa Moshi ulipata hadhi ya kuwa Manispaa mnamo mwaka 1988.
Ilikuwaje mpaka wahamiaji hao walipaona Moshi ni pazuri kuliko maeneo mengine nchini Tanzania hasa ikizingatiwa hata katika masuala ya kidini, wamisionari kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo walianzia mjini Moshi kisha kutawanyika kwenda maeneo mengine nchini.
Manispaa ya Moshi imezungukwa na Wilaya ya Moshi Vijijini kwa upande wa kusini, mashariki na kaskazini, wakati upande wa magharibi imepakana na Wilaya ya Hai.
Mji wa Moshi una eneo la kilometa za mraba 58, na upo kati ya mwinuko wa mita 700 Kusini hadi 950 Kaskazini kutoka usawa wa bahari.
Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa Halmashauri saba za Mkoa wa Kilimanjaro.
Wajerumani walipofika katika Kilimanjaro waliliona eneo la Tsudunyi, Kolila ambalo lipo Old Moshi (Moshi Vijijini) kwa sasa kama sehemu muhimu ya kuweka makazi yao hapo mnamo mwaka 1892.
Hata hivyo, baadaye mnamo mwaka 1911 walianza kuhamia taratibu katika eneo ambalo waliliita ‘Moshi Mpya’ au ‘New Moshi’ au kwa Kijerumani “Neu Moschi” ambapo watumiaji walianza kulitumia zaidi Moshi badala ya New Moshi na hadi leo panaitwa Moshi na kule ambako Wajerumani walianzia kunafahamika kwa jina la Old Moshi.
Ni ukweli usipopingika kwamba Kilimanjaro ndilo eneo maarufu zaidi Tanganyika kutokea Pwani, huku Mangi Rindi Mandara na Sultan wa Zanzibar wakiwa watawala mashuhuri zaidi waliofahamika barani Ulaya katika karne ya 19. Taasisi nyingi za mwanzoni za kiserikali na kidini Kaskazini ya Tanganyika zilianzia Moshi.
Baada ya Mangi Rindi Mandara kufariki, Wajerumani ambao walikuwa wameshajipanga walibadilika na kuanza kuwa wababe wakati huo Gavana wa Kijerumani Kilimanjaro akiwa Dkt. Karl Peters na walijenga kituo cha kijeshi Old Moshi mnamo mwaka 1892.
Hata hivyo, Umangi wa Old Moshi ulikuwa umerithiwa na Mangi Meli Mandara (mtoto wa Mangi Rindi Mandara) ambaye alikuwa jeuri na mwenye kujiamini sana na hakutaka kuwa chini ya utawala wa Wajerumani.
Kwa hali hiyo, hakukuwa na maelewano mazuri kati yake na Wajerumani na hata Wajerumani na watu wa Old Moshi kwa ujumla ambao walikuwa wajeuri sana dhidi ya ubabe wa Kijerumani.
Wakati huo huo, Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu aliimarisha mahusiano yake na Dkt. Karl Peters kiasi cha kumzawadia binti mrembo sana aliyeitwa Ndekocha na hivyo Karl Peters aliamua kuhamisha ofisi za utawala za Wajerumani Kilimanjaro kutoka Old Moshi, Tsudunyi kuhamia Marangu, Lyamrakana.
Gavana mpya aliyekuja Kilimanjaro Von Bulow hakuwa na maelewano mazuri na Mangi Ndegoruo Marealle licha ya kuishi Marangu na ubabe wake ulisababisha Von Bulow kuingia kwenye mzozo na hatimaye kulitokea vita kali iliyomfanya Von Bulow kukimbilia Kahe ambako aliuawa na askari watiifu kwa Mangi Mengi.
Alikuja kiongozi mwingine wa kijeshi kutoka Ujerumani aliyefahamika kwa jina la Kapteni Johannes ambaye alifanikiwa kuzirudisha ofisi za utawala kutoka Marangu ili awe na udhibiti wa Old Moshi.
Hapo ndipo Mji wa Moshi ukarudi upya eneo hilo la Tsudunyi na Ofisi za utawala Kilimanjaro kuanzia mwaka 1893 hadi 1919.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, Mji wa Moshi wenyewe ambao ulianzia Old Moshi na baadaye karne ya 20 kuteremka Moshi Mjini ulikuwa ndio mji mama Kaskazini ya Tanganyika ambapo ndio ulikuwa Ofisi za Utawala wakati huo “Wider Kilimanjaro” eneo lililokuwa linaanzia Usambara mpaka Arusha.
Kinachodhihirisha kuwa mji wa Arusha ulikuwa bado hata kabla ya Moshi ni mwaka 1899 pale Wachagga walipoungana pamoja na kwenda kuvamia Wamasai Arusha kuwakomboa baadhi ya ndugu zao waliokuwa wamechukuliwa mateka Umasaini, sambamba na kupora mali nyingi za Wamasai. Wakati huo Mji wa Moshi ulishaanza wakati ukiwa Old Moshi na Arusha ilikuwa ikitawaliwa kutokea Moshi na Wajerumani.
Katika suala la taasisi za dini zilizo nyingi zilianzia mjini Moshi, Kilimanjaro. Kwa mfano, Misheni ya Kilutheri ilianza kufungua vituo sita vya Nkwarungo, Machame, Ashira, Kidia, Siha, Masama na Mwika kabla ya kwenda kufungua misheni Arusha.
Miaka 15 baadaye ndipo misheni za Ilboru na Nkoaranga huko Arusha zilianzishwa zikiwa kama matawi ya Misheni ya Kilutheri Kilimanjaro.
Pia Misheni ya Kanisa Katoliki baada ya Zanzibar na Bagamoyo moja kwa moja walikuwa wakijiimarisha Kilimanjaro kabla hawajazidiwa na Waprotestanti maeneo mengine.
Mnamo mwaka 1912 Reli iliyokuwa inajengwa ikitokea Tanga kuelekea Kilimanjaro ilifika katika tambarare za Moshi Mjini na taratibu ukaanza Mji Mpya ambao uliitwa “The New Moshi” yaani Mji Mpya wa Moshi.
Mwaka 1919 Ofisi za Utawala Kilimanjaro pamoja na taasisi zake kama Hospitali ya Mawenzi, Mahakama na kadhalika vilivyokuwa Old Moshi, zilihamishiwa katika tambarare hizo ambazo zilikuwa mapori, pia hakukuwa na hali ya hewa nzuri.
Ndipo mwaka 1923 mchakato wa kuwa mji mdogo ukaanza ambapo kule mlimani ukapewa jina jipya “The Old Moshi” na mpaka leo panaitwa Old Moshi.