*Itahusisha sekondari 5,546 Tanzania Bara
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
WANAFUNZI wa kidato cha pili, leo Novemba 1, 2023 wanatarajia kuanza mitihani ya kijipima wa kitaifa (FTNA) hadi Novemba 9, 2023.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dkt. Said Mohamed alisema mitihani hiyo itafanyika katika shule za Sekondari 5,546 Tanzania Bara.
Alisema dhana ya upimaji kitaifa hutofautiana na ile ya Mitihani ya Taifa, upimaji wa kitaifa hufanywa katikati ya mafunzo wakati mitihani ya kitaifa hufanyika mwishoni mwa mafunzo.
“Wanafunzi 759,573 wamesajiliwa kufanya upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, 2023, wavulani 353,807 sawa na asilimia 46,58, wasichana 405,766 sawa na asilimia 53.42,” alisema.
Alieleza kuwa, wanafunzi wenye mahitaji maalum wapo 290, wenye ulemavu wa kusikia 309, wenye ulemavu wa viungo vya mwili 18.
Maandalizi ya upimaji huo yamekamilika, umuhimu wa mitihani hiyo ni kupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika mambo waliojifunza kipindi cha miaka miwili ya masomo yao ya sekondari.
Dkt. Mohamed alihimiza usalama kwenye vituo vya mitihani, vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na NECTA.
“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kuwa makini, wawe waadilifu ili kila mwanafunzi apate haki yake,”alisema .
Aliwataka wahakikishe wanafunzi wenye mahitaji maalum wanafanya upimaji wao ipasavyo ikiwemo kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.
Alisema wanafunzi wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa katika masomo mwengine kama mwongozo wa Baraza unavyoelekeza.
“Baraza linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa ili kuhakikisha upimaji wa kidato cha pili 2023 unafanyika kwa amani na utulivu,” aliongeza.
Wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano ili kudhibiti vitendo vyote vya udanganyifu katika upimaji huo na kwamba baraza halitasita kumchukulia hatua mtu atakayebainika kusababisha udanganyifu.