Na Daniel Mbega,
Kisarawe
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imezidi kung’ara kutokana na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo miradi 17 ya kielelezo kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Katika bajeti inayoishia Juni 30, 2023, Serikali ilipanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 15,521.3 (shilingi trilioni 15.52) kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kiasi cha fedha ambacho ni sawa na asilimia 37.8 ya bajeti yote ya taifa kwa mwaka huo wa fedha.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 12,122.1, sawa na asilimia 78.1 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za ndani na shilingi bilioni 3,399.2, sawa na asilimia 21.9 ya bajeti ya maendeleo ni fedha za nje.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ugharamiaji wa Mpango huo kama vilivyoainishwa katika Mkakati wa Ugharamiaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, malengo yakiwa ni Kuchochea Uchumi wa Ushindani na Shirikishi; Kuimarisha Uzalishaji Viwandani na Uwezo wa Utoaji Huduma; Ukuzaji wa Biashara na Uwekezaji; Kuchochea Maendeleo ya Watu.
Miradi 17 ya kipaumbele kwa mwaka 2022/23 ilikuwa ni; Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), na hususan reli ya Mtwara-Mbamba Bay na michepuo yake ya Mchuchuma na Liganga; Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP); Kuboresha Shirika la Ndege (ATCL); Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda; na Mchakato wa ujenzi wa Mtambo wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) mkoani Lindi.
Miradi mingine ni Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka; Mradi wa Makaa ya Mawe na Chuma wa Liganga; Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Ruhudji mkoani Njombe; Mradi wa Umeme wa Maji wa Rumakali mkoani Njombe; Ujenzi wa Madaraja na Barabara Kuu; Bandari ya Uvuvi ya Kilwa na Boti za Uvuvi; Kilimo cha Miwa na Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafiti wa Mafuta na Gesi katika bonde la Eyasi-Wembere; Utafiti wa mafuta na gesi katika bonde la Mnazi Bay Kaskazini; Ujenzi wa Kongani za Uchumi ikiwemo Bagamoyo; Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda Dodoma; na Kuendeleza Rasilimali Watu kwa maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule 26 za wasichana katika mikoa yote.
Utekelezaji wa miradi
Wakati akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/24, Waziri wa Fedha Dkt. MMwigulu Nchemba, alisema katika mwaka 2021/22 na robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na shughuli nyingine katika maeneo ya kipaumbele yaliyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
Akasema, katika kipindi hicho Ujenzi wa Reli ya Kati kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) ulikuwa umefikia asilimia 97.41 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 89.07; na kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) asilimia 12.53.
Aidha, Kipande cha Makutopora – Tabora (km 371) na kipande cha Tabora -Isaka (km 163) tayari vilikuwa vimepata mkandarasi na ufadhili, na kipande cha Tabora – Kigoma (km 514) na Uvinza – Malagarasi kuelekea Msongati (Burundi) – Gitega – Kindu (DRC) vilikuwa katika hatua ya kupata makandarasi.
Jumla ya shilingi trilioni 1.38 zilitumika kugharamia mradi huo katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 255.42 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Kuhusu kuliboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hadi wakati huo malipo ya awali ya ndege tano (5) yalikuwa yamekamilika ambapo ndege nne ni za abiria na moja ya mizigo.
“Jumla ya Shs. 732.56 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 494.61 milioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23,” akasema.
Mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shs. 360 bilioni na uwekaji wa jiwe la msingi ulifanywa mwezi Novemba 2022.
Akasema, ukamilishaji wa taratibu za fedha kwa ajili ya viwanja vya ndege Kigoma, Tabora, Shinyanga na Rukwa zinaendelea.
Kuhusu Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115), hadi kufikia Oktoba 2022 utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 75 ambapo jumla ya Shs. 1.273 trilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 394.02 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Aidha, Serikali imeendelea na usambazaji wa umeme vijijini (REA) ambapo vijiji 9,163 kati ya vijiji 12,345 vya Tanzania Bara vimeunganishiwa umeme. Jumla ya Shs 313.40 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 84.90 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Serikali pia imekamilisha malipo ya fidia kwa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani – Tanga (Tanzania) – EACOP katika maeneo 14 yatakayojengwa kambi za wafanyakazi, hifadhi za vifaa na karakana.
Vilevile, ujenzi wa kiwanda cha kupaka rangi kwenye mabomba unaendelea, na Serikali imekwishatoa jumla ya Shs. 261.33 bilioni ikiwa ni sehemu ya malipo ya 15% ya umiliki wa Serikali katika mradi. Jumla ya Shs. 224.69 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 36.63 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) – Lindi, majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) kati ya Serikali na Wawekezaji kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi wa masuala ya sheria, fedha, biashara, uchumi na masoko bado yanaendelea, ambapo Shs. 3.69 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 963.0 milioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Serikali inaendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini chini ya usumamizi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) kwa kujenga barabara za mikoa na barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na barabara za mijini na vijijini.
Katika kipindi hicho, ujenzi wa madaraja ya Tanzanite (Dar es Salaam), Kiyegeya (Morogoro) na Ruhuhu (Ruvuma) umekamilika.
Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66 ambapo ujenzi umefikia asilimia 47.32, Daraja la Wami (Pwani) na barabara unganishi (km 3.8) asilimia 83 na kuanza kutumika katika kipindi cha uangalizi, daraja la Kitengule (Kagera) na barabara unganishi (km 18) asilimia 95.15 na daraja la Sibiti (Singida) asilimia 95.15.
“Kwa ujumla ya miradi 14 ya barabara zenye urefu wa kilometa 883 imekamilika kati ya Aprili 2021 hadi sasa, yaani ndani ya kipindi cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ya Shs. 1.37 trilioni.
“Pamoja na hayo kuna jumla ya miradi 44 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,523 yenye gharama ya Shs. 3.8 trilioni ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi nchi nzima,” alisema Mwigulu katika hotuba yake.
Vilevile, miradi 62 ya barabara iko katika hatua mbalimbali za manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Utekelezaji wa Miradi kwa kutumia utaratibu wa EPC + F mchakato wake umekwishaanza kwa Miradi 8 yenye urefu wa kilometa 2,533 na hatua za kimanunuzi zinaendelea. Aidha, jumla ya miradi 43 ya barabara yenye jumla ya urefu wa kilometa 2,021.04 ipo kwenye hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa gharama ya jumla ya Shs. 9.6 bilioni.
Kuhusu ujenzi wa barabara na madaraja chini ya usimamizi wa Tarura, Mwigulu alisema kwamba mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 275.85, changarawe kilometa 11,120.89, madaraja 596, makalavati na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 67.44 ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa matengenezo ya kawaida ya barabara zenye jumla ya kilometa 25,078.73.
Akabainisha kwamba, jumla ya Shs. 2.36 trilioni zimetumika katika ujenzi wa barabara na madaraja kwa mwaka 2021/22 na Shs. 670.46 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Aidha, kwa kupitia bajeti ya mwaka 2022/23 jumla ya zabuni 1,706 zenye thamani ya Shs. 621.66 bilioni zimetangazwa na Tarura ambapo kati hizo Wakala imekwishaingia jumla ya mikataba 1,246 na Wakandarasi kwa kazi mbalimbali kwa nchi nzima yenye thamani ya Shs. 406.21 bilioni.
Kazi za mikataba hiyo, alisema, zimeshaanza na zinaendelea na zinahusisha ukarabati, ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja makubwa matatu ya Berega (Kilosa) lenye urefu wa Mita 140, Msadya (Mpimbwe-Katavi) lenye urefu wa Mita 60, na Mkomazi (Korogwe) lenye urefu wa
Mita 40, madaraja ambayo yanaunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo.
Uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga unaendelea ambapo jumla ya Shs. 328.56 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 19.95 bilioni zimetumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Kwa upande wa Kilimo, kwa kutumia mfumo maalum wa utambuzi unaotumia QR Code, Serikali imeratibu uuzaji wa mbolea ambapo kufikia tarehe 5 Novemba, 2022 tani 67,296 za mbolea zenye thamani ya ruzuku ya Shs. 74.47 bilioni zimenunuliwa na wakulima kwa kutumia mfumo maalum.
Aidha, Serikali inaendelea na zoezi la usajili wa wakulima kwa kutumia alama za vidole (biometric registration) ambapo kufikia tarehe 5 Novemba, 2022 wakulima 2,118,911 wamesajiliwa kwenye mfumo huou.
Serikali ilitoa Shs. 29 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za Korosho na kutolewa ruzuku ya mbegu na viatilifu vya pamba vyenye thamani ya Shs. 75 bilioni.
Kwa upande wa Kilimo cha Umwagiliaji, hadi kufikia mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 jumla ya Mikataba 21 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye skimu za kijamii yenye thamani ya Shs. 182 bilio ni imesainiwa na wakandarasi wako uwandani (site).
Serikali imekamilisha ujenzi wa majosho 192 katika mamlaka za Serikali za Mitaa 85, kuzalishwa kwa jumla ya dozi 50,261 za mbegu za mifugo, kukamilika kwa ujenzi wa minada nane (8) na ukarabati wa minada tisa (9); kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa ya Chamakweza (Pwani), Kimambi (Lindi) na Mhanga (Singida); na kuanzishwa kwa program ya vituo atamizi (SAUTI Program = Samia Ufugaji kwa Tija
Program) katika vituo 8 na kila kituo kuwa na vijana 30, ambao tayari wamesharipoti kwenye vituo hivyo na kuanza kutengeneza miundombinu inayohitajika kwa ufugaji kwenye vituo hivyo.
Kwa upande wa Afya, serikali inaendelea kukamilisha ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa 19; kuendelea na ujenzi wa Hospitali 135 za Halmashauri ambapo hospitali 70 zimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje;vituo vya afya 335 na zahanati 668, kununuliwa na kusambazwa kwa chanjo mbalimbali; na kufungwa kwa mitambo 19 ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni katika hospitali za rufaa za mikoa na mitambo 13 katika Hospitali za Wilaya ambapo jumla ya Shs. 563.85 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 75.32 bilioni katika robo
ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji ambapo hadi Juni 2022 umefikia wastani wa asilimia 74.5 vijijini kutoka asilimia 72.3 Juni 2021 na mijini asilimia 86.5 kutoka asilimia 86 mwaka 2021.
Miradi 394 imekamilika ambapo wananchi wapatao 1,336,856 waishio vijijini wamenufaika; na miradi 145 imetangazwa ili kupata wakandarasi wa ujenzi.
Aidha, Miradi ya maji katika miji 28 imeanza utekelezaji baada ya kupatikana wakandarasi; mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidunda amepatikana; na mtaalam mshauri kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Farkwa amepatikana. Kupitia mradi wa Uviko-19, seti 25 za mitambo ya uchimbaji visima zimenunuliwa, seti 5 za mitambo ya uchimbaji na ujenzi wa mabwawa zimenunuliwa, miradi 154 ya maji vijijini na 42 mijini imeanza kutoa huduma kwa wananchi na utekelezaji wa miradi 18 ya maji vijijini na minne (4) ya mijini unaendelea na umefikia wastani wa asilimia 97. Jumla ya Shs. 598.5 bilioni zimetumika katika mwaka 2021/22 na Shs. 74.35 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.
Kwa upande wa Elimu, Serikali imeendelea kutekeleza programu ya Elimumsingi Bila Ada ambapo jumla ya Shs 296.46 bilioni zimetolewa n kuendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,425 (sekondari 1,295 na msingi 2,130).
Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya Shs. 569.0 bilioni kwa wanafunzi 177,925 wa Elimu ya Juu; na kukamilika kwa ujenzi wa madarasa mapya 15,000 (madarasa 12,000 kwa ajili ya shule za sekondari na madarasa 3,000 kwa ajili ya shule za msingi) na mabweni 50 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 25 na vyuo vinne vya watu wenye ulemavu kupitia mradi wa Uviko-19.
Ukamilishaji wa madarasa uliwezesha wanafunzi wote 907,802 waliofaulu darasa la saba kuingia kidato cha kwanza mwaka 2022 bila kuwepo kwa awamu za kusubiria.
“Kwa mwaka huu tayari tumetoa Shs. 160 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8,000 ya kuanzia, bado tunatafuta fedha za madarasa mengine 8,000 ili kupata madarasa 16,000 ya kuweza kutosheleza matarajio ya watoto wengi zaidi kujiunga na mwaka mpya wa masomo ya Sekondari. Jumla ya Shs. 1,187.56 bilioni zimetumika katikamwaka 2021/22 na Shs. 274.39 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23,” alisema Mwigulu.