Mil 900/- za Betika zilivyonogesha Mbeya Tulia Marathon

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

KAMPUNI namba moja ya Michezo ya Kubashiri Tanzania ya Betika, imenogesha mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon kwa udhamini wa sh. milioni 900.

Msimu huu, mbio hizo zimedhaminiwa na Betika imefanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Ijumaa na Jumamosi iliyopita na kutoa upinzani mkali kwa wanariadha wa mbio fupi za uwanjani waliochuana Ijumaa na nyota wa barabarani (marathon na nusu marathon) wakihitimisha ngwe ya msimu huu.

Katika kuendelea kunogesha mbio hizo zimezoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson na Spika wa Bunge, alipokea hundi ya sh. milioni 900 kutoka kwa wadhamini wa mbio hiyo, Kampuni ya Betika.

Kwa upande wa Meneja Mkuu wa Betika Tanzania, Samuel Mucheru, amesema udhamini huo ni wa miaka mitatu kuanzia mwaka huu, 2026 na mwaka 2027.

“Betika tunayo furaha kuungana na Taasisi ya Tulia Trust kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ya elimu na afya sambamba na kukuza michezo kupitia mbio hizi,” amesema Mucheru.

Akizungumzia udhamini huo, Dkt. Tulia amesema fedha inayokusanywa katika mbio hizo zinakwenda kuendeleza lengo la mbio hizo inayogusa jamii katika nyanja ya elimu, afya na kusaidia wazee wasiojiweza.

Katika afya, Dkt. Tulia amesema wametoa bima za afya kwa wananchi 9,000.

Pia kwenye elimu mbali na kuboresha miundombinu, wanawezesha mahitaji kwa watoto wanaotoka kwenye kaya maskini ikiwamo kuwapa sare za shule na madaftari.

“Pia tunazifikia kaya za wazee wasio jiweza kwa kuwajengea makazi bora na mahitaji mengine kama chakula na mavazi, ili kuwapa faraja wenzetu,” amesema.

Akifunga mbio hizo msimu huu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, amesema mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon mbali na kusaidia kuboresha elimu na afya na kukuza mchezo, pia inatoa fursa kwa wafanya biashara mkoani Mbeya.

Dkt. Biteko aliyekuwa miongoni mwa wakimbiaji wa mbio ya kilomita tano sanjari na Dkt. Tulia, Meneja Mkuu wa Betika Tanzania, Samuel Mucheru, Rais wa Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi na viongozi wengine wa chama na Serikali alisisitiza umoja na ushirikiano kupitia mbio hizo.

Amesema mbio ya Betika Mbeya Tulia Marathoni ilipoanza kuna watu waliibeza.

“Leo hii ni mbio kubwa na ya kipekee nchini ambayo imejitofautisha na zingine, ikifanyika siku mbili mfululizo na wafanyabiashara wananufaika nayo, wanariadha wananufaika nayo pia huku ikiendelea kuunga mkono mikakati ya Serikali katika kuboresha miundo mbinu ya elimu na afya, ili ni jambo kubwa na la mfano,” amesema.

Mbio hizo ni mbio pekee ya marathon nchini inayofanyika kwa siku mbili, ikishindanisha wanariadha wa mbio fupi za uwanjani za meta 100, 200, 400, 800 na 1500 sambamba na mbio za meta 50 kwa watoto katika siku ya kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *