Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali, majimbo, wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wa halmashauri kutoelewana kwenye utendaji kazi wao.
Alisema hali hiyo inadhoofisha utendaji na maendeleo ya Serikali, mikoa na halmashauri kutokana na baadhi ya viongozi hao kutoelewana.
Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar, jana wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wawili na wakuu wa Wilaya watatu aliowateua hivi karibuni.
Aliwaonya baadhi ya viongozi wasioshughulikia kero za wananchi na wanaojihusika na kero hizo akiwatka wafanye kazi ya kuwatumikia wananchi, kutenda haki badala ya kuwa sehemu ya kero hizo.
“Kazi yenu ni kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yenu, wananchi wanachangamoto nyingi, kabla ya kuzifikisha ngazi za juu mhakikishe kwenu zimeshindikana,” alinasihi Rais Dkt. Mwinyi.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, Rais Dkt. Mwinyi alisema imekua tatizo kubwa hasa kwa baadhi ya viongozi kujihusisha na kero hizo.
Aliwaasa viongozi hao kuhakikisha wanatatua kero hizo na kutenda haki kwa wananchi badala ya kuwaachia hadi kufikisha malaalmiko yao ngazi za juu serikalini.
Kuhusu kero za wawekezaji, alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa mikoa na Wilaya kutatua kero za wawekezaji kwenye ngazi zao kwa kuwatendea haki badala ya kuwapendelea au kuwadhulumu.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuwasimamia vema waliochini yao hasa Halmashauri za Wilaya na manispaa zao kuhusu wajasiriamali wadogo, kushughulikia usafi wa mazingira bila kuiachia serikali.
Rais Dkt. Mwinyi alikemea uhusiano mbaya baina ya viongozi wa Serikali, mikoa, wilaya wakiwemo Mawaziri, mawakili, wabunge majimboni pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.
Aliwataka viongozi wote kufanya kazi pamoja, kushirikiana na kuelewana,kuonya tabia ya kususiana kwenye majukumu yao jambo linalodhoofisha utendaji kazi wa serikali na kuonya kuwa, kama tabia hiyo haitaachwa, atalazimika kuchukua hatua.
Rais Dkt. Mwinyi aliwataka Wakuu wa mikoa na Wilaya zote za Zanzibar, kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwenye suala la ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Baadhi ya maeneo kumeripotiwa matukio mengi ya uvunjifu wa amani hasa maeneo ya Paje Mkoa wa Kusini Unguja na Nungwi, Kaskazini Unguja hivyo aliwataka viongozi hao kuyashughulikia matukio hayo.
Pia aliwataka waendeshe operesheni maalum ya kudhibiti hali hiyo isitokee kwenye maeneo hayo ambapo Serikali imeweka nguvu kubwa ya Utalii.
Walioapishwa ni Ayoub Mohamed Mahmoud kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, awali alikua Mkuu wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, awali alikua Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Sadifa Juma Khamis kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja, kabla alikua Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja. Othman Ali Maulid kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, awali alikua Mstaafu kutoka Utumishi wa Umma.
Pia Rais Dkt. Mwinyi alimuapisha Galos Nyimbo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, kabla ya hapo Galos alikua mwanajeshi mstaafu.