Miaka 12 baada ya Ban Ki Moon, Samia ahutubia Bunge la Zambia

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatano, Oktoba 25, 2023, anahutubia Bunge la Taifa la Zambia ikiwa ni miaka 11 na siku 243 (takriban miaka 12) tangu Bunge hilo lilipohutubiwa na kiongozi wa kigeni.

Ilikuwa Ijumaa, Februari 24, 2012 wakati Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alipohutubia Bunge la Zambia wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini humo, ikiwa ni miezi michache tu baada ya Michael Satta wa chama cha Patriotic Front kuingia madarakani bada ya kumshinda Rupiah Banda kwenye uchaguzi wa mwaka 2011.

Yeye ndiye Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhutubia Bunge la Zambia.

Ki Moon alihutubia Bunge hilo takriban siku 12 baada ya Timu ya Taifa ya Zambia, Chipolopolo, kunyakua kwa mara ya kwanza taji la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Libreville nchini Gabon.

Ndiyo maana katika hotuba yake, Ki Moon aliipongeza timu hiyo kwa kuweka historia ya pekee licha ya kukabiliana na timu ngumu kwenye michuano hiyo.

Namnukuu: “…Nimekuja nikibeba ujumbe wa maneno mawili kwa Zambia kutoka ulimwenguni: Hongera. Chipolopolo! Ushindi ulioje! Afrika na dunia iliona zaidi ya mafanikio ya timu ya soka. Tuliona ari ya Zambia katika ushindi wa soka wa Kombe la Mataifa ya Afrika.

“Wote wanaoamini miujiza, wote wanaoanzisha mashujaa wasiojulikana, wote wanaoheshimu wale waliotangulia, tunajua: ushindi wa Zambia uliandikwa angani. Naamini ushirikiano wetu umeundwa na roho hiyo hiyo kubwa…” – Mwisho wa kunukuu.

Na kwa kweli Chipolopolo walikuwa wanastahili kupongezwa kutokana na jitihada kubwa walizozionyesha mwaka huo wakati mashindano yalipoandaliwa kwa ushirikiano baina ya Gabon na Guinea ya Ikweta.

Walipoifunga Senegal 2-1 kwenye hatua ya makundi, hakuna aliyeamini, lakini walipoendelea kuwadonoa wapinzani na kutinga fainali kukutana na Ivory Coast wengi wakasema ndio mwisho wao.

Kwamba, kama akina Kalusha Bwalya walishindwa kuonyesha maajabu kipindi kile wako juu hata baada ya ajali iliyoua kikosi kizima, hawa vijana wadogo wangeweza wapi!

Lakini mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade d’Angondjé, Libreville Februari 12, ulishuhudia timu hizo zikitoka suluhu katika dakika zote 120, hivyo kuingia kwenye mikwaju ya penalty.

Zambia ikashinda kwa penalty 8–7, huku bwanamdogo Stophira Sunzu aliyekuwa akiichezea TP Mazembe akifunga penalty ya ushindi. Kaka yake, Felix Sunzu Jr, wakati huo alikuwa akiicheza Simba ya Dar es Salaam iliyomsajili kutoka Al Hilal ya Sudan.

Yosso wa Zambia akina Kennedy Mweene, Davies Nkausu, Stophira Sunzu, Hijani Himoonde, Joseph Musonda, Chisamba Lungu, Isaac Chansa, Nathan Sinkala, Rainford Kalaba, Emmanuel Mayuka, Felix Katongo na nahodha Christopher Katongo, hawakutishwa na majina makubwa ya akina Boubacar Barry, Jean-Jacques Gosso, Kolo Touré, Sol Bamba, Siaka Tiéné, Didier Zokora, Yaya Touré, Cheick Tioté, Gervinho, Salomon Kalou, Wilfried Bony, Max Grdel, Didier Ya Konan na nahodha Didier Drogba, ambao karibu wote walikuwa akicheza kwenye ligi kubwa Ulaya.

Naam. Ki Moon alikuwa na kila sababu za kuwapongeza Zambia kwa mambo makubwa waliyoyafanya kwenye mashindano hayo.

Lakini leo hii Rais Samia anapolihutubia Bunge la Zambia watu hawaangalii mafanikio katika michezo, bali wanaangalia, pamoja na mambo mengine, msuala ya ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia pamoja na ukuzaji wa uchumi.

Kimsingi hotuba ya Rais Samia kwenye Bunge hilo ni ya kihistoria, kwani ndiye kiongozi pekee wa kigeni wa kike kuhutubia chombo hicho cha kutunga sheria.

Usawa wa jinsia                            

Kwa bahati pia, Rais Samia ni kiongozi wa kwanza wa kigeni kuhutubia Bunge la 13 la Zambia likiwa chini ya Spika mwanamke, Mwanasheria Nelly Butete Kashumba Mutti aliyechaguliwa Septemba 3, 2021 akichukua nafasi ya Patrick Matibini, ambaye aliondoka madarakani baada ya uchaguzi wa Agosti 12, 2021 ulioshuhudia Rais Edgar Lungu akiangushwa na Hakainde Hichilema.

Hii inadhihirisha namna Zambia nayo inavyojitahidi kuwapa nafasi wanawake kwenye maamuzi, hatua ambazo zilikwishachukuliwa na kitambo na Tanzania, ambayo kwa mara ya pili Bunge linaongozwa na Spika mwanamke, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu.

Nelly Mutti, mwanasheria aishiye jijini Lusaka, alichaguliwa bila kupingwa na wabunge wote 166 wa Bunge la Zambia.

Nelly (67) amekuwa Spika wa 6 wa Bunge la Zambia tangu nchi hiyo ilipopata uhuru Oktoba 24, 1964, lakini ni Spika wa nane tangu cheo hicho kilipoanzishwa kwenye Bunge hilo mwaka 1948 wakati wa ukoloni wa Mwingereza, wakati huo ikijulikana kama Rhodesia ya Kaskazini.

Maspika waliomtangulia baada ya Uhuru ni Wesley Nyirenda (1964-1968), Robinson Nabulyato (1968-1988, na 1991-1998), Fwanyanga Mulikita (1988-1991), Amusaa Mwanamwambwa (1998-2011), Patrick Matibini (2011-2021).

Kuanzia Novemba 10, 1948, cheo hicho kilishikwa na watu wawili – Thomas Spurgeon Page (1948-1956) na Thomas Williams (1956-1964). Kabla ya hapo, Gavana ndiye pia alikuwa na cheo cha Spika wa Baraza la Kutunga Sheria.

Matarajio

Matamanio ya Wazambia na Watanzania ni kusikia kilichomo kwenye hotuba ya Rais Samia kwenye Bunge hilo, ingawa wengi wana matumaini makubwa kwamba, itajikita kwenye kuimarisha uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia ina changamoto kadha wa kadha zikiwemo za ukame unaosababisha baa la njaa pamoja na majanga ya vita kama vile vya Ukraine na Urusi na mgogoro wa Israel na Paletina.

Kupanda kwa bei ya mafuta kulikosababishwa na kupungua kwa uzalishaji wa nishati hiyo kutoka nchi wanachama wa OPEC+ kumeongeza gharama ya maisha kwa wananchi wa pande zote mbili, huku Zambia ikikumbwa na mfumuko mkubwa wa bei uliosababisha kushuka kwa thamani ya sarafu yake, Kwacha.

Jana Rais Samia, ambaye yuko nchini Zambia kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, alihutubia kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia ambazo pia zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.

Rais Samia pia alialikwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia, ambalo lilianza jana jijini Lusaka.

Ziara hii ni ya kwanza ya Kitaifa ya Rais kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022.

Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umejengwa na misingi ya kindugu, hivyo ziara hiyo imelenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu ambapo Rais Samia na mwenyeji wake walijadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la Tazama, Reli ya Tazara na Barabara ya TanZam.

Malengo mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha  shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza  jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika  katika bandari ya Dar es Salaam.

Aidha, ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.

Ni dhahiri kwamba, baada ya ziara hii, kuna mafanikio makubwa yanayoweza kutokea, hasa ikichukuliwa kwamba, tayari Tanzania imekwishaingia mikataba ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya DP World ya Dubai, hiyo kuongeza ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *