Na Anita Nkonge, Alfatih Wadidi na Priya Sippy
BBC
MZOZO ulioanza katikati ya mwezi Aprili mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka umeufanya mfumo wa elimu wa nchi hiyo kufikia ukingo wa kuporomoka.
Zaidi ya shule 10,000 zimefungwa, huku zaidi ya shule 170 zinatumika kama makaazi ya dharura kwa wale waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano.
Jaafar Abbakar, mzazi wa watoto wanne, ni mmoja wa wale wanaoishi katika makazi ya shule. Yeye na familia yake walikimbilia jimbo la Gederaf kutoka Umbada, magharibi mwa Omdurman. Anasema hata kama shule zitafunguliwa mwaka huu, watoto wake hawako tayari kurejea.
“Ni vigumu kwa sababu za kisaikolojia. Katika hali kama hizi, mtu hawezi kwenda shule. Hakuna dalili za kuahidi kwamba vita vitaisha,” anasema.
“Lazima kuwe na amani na utulivu nchini ili watu wafanye biashara zao wakiwa na afya, ndipo mwaka wa shule uanze.”
“Ninajaribu kuwasomesha iwezekanavyo. Hatuwezi kufanya mengi, lakini tunafanya kile tunachoweza ingawa sio endelevu. Tunajaribu kuwadurusisha nyumbani ili wasahau madhara ya vita,” anasema.
Binti yake mwenye umri wa miaka 15, Eram, anawakosa marafiki zake wa shule. “Baada ya kutengana, hakukuwa na mawasiliano kati yetu,” anasema.
Unicef inakadiria hata kabla ya vita kuzuka karibu watoto milioni saba walikuwa tayari hawaendi shule nchini Sudan kutokana na umaskini na ukosefu wa utulivu. Sasa watoto zaidi ya milioni sita na nusu hawaendi shule kutokana na mapigano – huku zaidi ya watoto milioni tano wameathiriwa na kufungwa kwa shule.
“Watoto hawawezi kwenda shule kwa sababu ya vurugu. Pia wako katika hatari ya unyanyasaji wa kingono, kijinsia na wanahitaji ulinzi wa kimwili na pia walimu,” anasema Yasmin Sherif, mkurugenzi mtendaji wa Education Cannot Wait.
Mgogoro unaoendelea sio jambo pekee ambalo limesukuma mfumo wa elimu kuporomoka. Janga la hivi karibuni la uviko 19 pamoja na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kufa kwa mfumo wa shule.
Wakati Baraza la Mawaziri la Sudan likisema vyuo vikuu na shule vinaweza kufunguliwa katika majimbo ambayo usalama unaruhusu. Kamati ya Walimu ya Sudan ilikataa kauli hiyo, ikisema masuala kadhaa yanahitaji kutatuliwa kwanza.
Ali Obaid, ni mwalimu anaye fanya kazi katika Wizara ya Elimu kwa zaidi ya miaka 28, yupo katika Kamati ya Walimu ya Sudan.
“Kuna vikwazo vingi vinavyokwamisha kufunguliwa kwa mwaka wa masomo, ikiwa ni pamoja na kupoteza mashule kutokana na uharibifu, uhamiaji na uhamisho wa wanafunzi na walimu, na taasisi nyingi za elimu zimegeuzwa kuwa vituo vya makazi,” anasema.
“Hata kabla ya Aprili, tulikuwa tukitaka mishahara iongezwe kwa sababu mishahara ya walimu ilikuwa miongoni mwa mishahara ya chini zaidi nchini. Mambo haya yote yametengeneza hali ngumu sana kwa mwalimu na kutuweka chini ya mstari wa umaskini,” anasema Obaid.
NGOs, kama vile Unicef, zimekuwa zikijaribu kusaidia watoto kuendelea na elimu nje ya shule, kupitia mipango kama vile majukwaa ya kujifunza ya mtandaoni.
Lakini, kulingana na Unicef, hatua hizi haziwezi kuchukuliwa kuwa mbadala wa elimu rasmi, na serikali inapaswa kufungua shule haraka iwezekanavyo.