Na Sarah Moses, Dodoma.
JUMLA ya Taasisi za Umma 109 zimeunganishwa katika Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB ) huku mifumo 117 ikiwa imesajiliwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Desemba 22,2023,jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Benedict Ndomba amesema kuwa miongoni mwa taasisi zilizosajiliwa ni pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Wakala wa Leseni za Biashara (BRELLA), na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Amesema kuwa mfumo wa GovESB umeleta mafanikio makubwa katika sekta za elimu na sheria kwani taasisi nyingi katika sekta hizo zinabadilishana taarifa kupitia GovESB.
Kwaupande wa sekta ya sheria,taasisi zinazobadilishana taarifa ni Mahakamani, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), nakusema kuwa mfumo huo umesaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, uwazi pamoja na utoaji haki kwa wananchi kwa wakati.
“Katika sekta ya elimu,taasisi zilizounganishwa na kubadilishana taarifa kupitia mfumo huu ni pamoja na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Chuo Kikuu cha Dar es Salama, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)” amesema Ndomba.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema ili kuhakikisha taasisi nyingi zaidi zinajiunga na mfumo wa GOvESB na kubadilishana na sekta, e-GA imekuwa na mikakati madhubuti ikiwemo kufanya vikao na taasisi mbalimbali ambayo kati ya Agosti na Novemba 2023,imefanya vikao na taasisi 55 .
Pamoja na hayo amesema kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo kulikuwa na changamoto mbalimbali kama kutumia muda mrefu kupata taarifa, utofauti wa utaratibu wa kupata taarifa kutoka taasisi moja hadi nyingine.
Wakati huo huo akizungumzia mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Ufundishaji wa Shehena maeneo ya Forodha (TeSWS) amesema e-GA imeshirikiana na taasisi nyingine za Umma kama TRA,TPA na Wizara ya Fedha katika kusanifu mfumo huo.
“Mfumo huu ni moja ya miradi inayotekelezwa chini ya mradi mkubwa wa kujenga uwezo wa kitaasisi wa kukusanya mapato ya ndani na usimamizi wa maliasilia (ISP-DRM-NRG) unaosimamiwa na Wizara ya Nishati” amesema.
Pia amesema mfumo wa TeSWS ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuboresha Wafanyabiashara kukamilisha maombi ya vibali na maandalizi ya malipo ya kodi za forodha kidijitali bila kwenda kwenye Taasisi mbalimbali za udhibiti wa forodha na hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Lakini pia mfumo huu unaruhusu wadau wa biashara na wasafirishaji kuwasilisha maramoja tu kwenye mfumo taarifa za ni forodha na shehena zinazoingia na kutoka nchi ni,pamoja na zile zinazopita nchi jirani ambayo kila mdau husika ataziona na kuzifanyia kazi kwenye mfumo.
Ndomba akizungumzia mfumo wa Ubadilishanaji wa Taarifa kati ya Mifumo ya TEHAMA ya Serikali na Sekta Binafsi amesema mfumo huo unawezeshwa kadri ya mahitaji yanavyojitokeza,mathalani mfumo wa malipo ya Serikali (GePG)umeunganishwa na Benki zote nchi ni pamoja na kampuni zote za Simu za mikononi ili kuwezesha huduma ya malipo ya Serikali kupitia Simu za mikononi.
“Mfumo wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi umeunganishwa na mifumo ya kampuni zote za simu nchini hivyo kuwezesha kutoka huduma za Serikali kwa njia ya simu za mkononi” amesema.
Mwisho.