FLORIDA, Marekani
NYOTA Lionel Messi, ametajwa kuwa bora duniani wakati akifunga bao lake la 10 katika mechi saba na kuisaidia timu yake ya Inter Miami kutwaa taji la kwanza.
Messi, 36, ambaye ni raia wa Argentina, alifunga bao nje ya eneo la hatari na kuipa bao la uongozi Miami dhidi ya Nashville SC katika fainali ya Kombe la Ligi.
Hata hivyo, Fafa Picault, aliisawazishia timu yake kipindi cha pili na mchezo kwenda katika mikwaju ya penalti.
Miami ilishinda kwa mikwaju 10-9 baada ya Drake Callender alipopangua penalti iliyopigwa na kipa wa Nashville, Elliot Panicco.
Miami ilikuwa na rekodi mbaya ndani ya Ligi Kuu ya Marekani msimu huu kabla ya ujio wa mshindi wa Kombe la Dunia, Messi kutua mwezi uliopita pamoja na wachezaji wenzake wa Barcelona, Jordi Alba na Sergio Busquets.
Hilo ni taji la kwanza kwa klabu hiyo tangu ilivyoanzishwa mwaka 2020.
Pia ina nafasi ya kutinga fainali nyingine wakati itakapoumana na Cincinnati katika nusu fainali ya US Open Cup Jumatano.