Mechi saba zamuondoa Kopunovic Pamba

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

UONGOZI wa timu ya Pamba Jiji FC, umetangaza kumfuta kazi Kocha, Goran Kopunovic ambaye amekiongoza kikosi hicho katika mechi saba za Ligi Kuu Bara msimu huu.

Katika mechi saba alizosimama kama kocha, Kopunovic hajapata ushindi katika mechi yoyote ikiwa wametoka sare mara nne na kufungwa mechi tatu.

Mbali na Kopunovic, lakini uongozi wa Pamba Jiji FC umetangaza kuwafuta kazi Kocha Msaidizi, Salvatory Edward na Kocha wa Makipa, Razaq Siwa.

“Katika kipindi hiki cha mpito timu yetu itakuwa chini ya Mathias Wandida ambaye ni kocha wetu wa kikosi cha U-20,” imesomeka taarifa ya Pamba Jiji FC.

Pamba Jiji ipo katika maandalizi ya mechi ya ligi mzunguko wa nane ambapo Jumapili watakuwa nyumbani kukabiliana na Kagera Sugar.

Mechi yao ya mwisho ya ligi chini ya Kopunovic waliicheza dhidi ya Yanga SC katika dimba la Azam Complex, Dar es Salaam ambapo walipoteza kwa kufungwa mabao 4-0.

Pamba Jiji FC imepanda kucheza ligi hiyo msimu huu baada ya kushuka daraja miaka 23 iliyopita. Hata hivyo urejeo wao bado haujakuwa na tija baada ya timu hiyo kushindwa kuvuna alama tatu hata mara moja katika mechi saba.

Kopunovic ambaye alitambulika zaidi nchini baada ya kujiunga na Simba, msimu uliopita aliifundisha timu ya Tabora United na kuondoka kabla ya msimu kuisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *