Mchengerwa awatahadharisha wanaoishi mwambao wa Pwani

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amewataka wananchi wanaoishi mwambao wa Pwani, kutumia maboti ya kisasa na kupunguza kutumia maboti ya asili hasa katika kipindi cha dhoruba pamoja na kuacha kubeba watu wengi kwenye mtumbwi mmoja.

Mchengerwa ameyasema hayo leo kufuatia vifo vya watu wanne na vilivyotokea katika mto Rufuji mkoani Pwani kwa ajali ya mtumbwi na wengine saba kujeruhiwa.

“Wananchi wote mnaokaa mwambao wa Pwani mtumie maboti ya kisasa na mpunguze kutumia maboti ya asili na kuacha kubeba watu wengi,”amesema.

Amesema ajali hiyo ilitokea Novemba 19, 2023 baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria wakitokea shambani kupinduliwa na kiboko kwenye Mto Rufiji, Kijiji cha Mloka, Kitongoji cha Mpanga.

“Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya, Edward Gowelle watu hao wanne waliofariki ni wa familia moja, majeruhi saba wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rufiji,”amesema.

Mchengerwa ametoa pole kwa majeruhi wa ajali hiyo na wafiwa wote na kuungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *