Mchengerwa aagiza usimamizi thabiti utekelezaji miradi ya TACTIK

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kuhakikisha miradi ya TACTIC awamu ya pili inayotekelezwa Jijini Arusha inakamilika kwa wakati na kuleta tija iliyokusudiwa katika kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi na wageni wanaotarajiwa kunufaika na huduma za manunuzi, huduma bora za usafiri na mazingira bora ya ufanyaji biashara.

Mchengerwa alibainisha hayo Mei 2, 2025, baada ya kushuhudia utiaji saini utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa Jijini Arusha chini ya Mradi wa TACTIC ambayo ni Ujenzi wa Kituo kikuu cha Mabasi, Ujenzi wa Soko kuu la Kilombero, Ujenzi wa soko la Morombo pamoja na Uboreshaji wa Bustani ya mapumziko ya Themi Living Garden, miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa miezi 15 kwa gharama ya Sh. bilionu 30.6 chini ya Mkandarasi M/s Mohammed Builders Limited.

“Mradi huu wa TACTIC tunaouzindua leo sio miundombinu tu bali ni daraja kati ya leo na kesho bora ya wananchi na ni kweli isiopingika kuwa maendeleo ya miji ni kioo cha ustaarabu wa nchi yetu, miundombinu bora ya usafiri na masoko ya kisasa na bustani ya kijani ni taswira ya jamii yetu, ” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa pia ametoa rai kwa wakuu wa mikoa na halmashauri zote nchini zinazotekeleza miradi ya TACTIC nchini kuandaa mipango mizuri ya kuhakikisha miradi ya masoko na vituo vya mabasi vinajiendesha vyenyewe na kuzalisha mapato, akitoa rai pia kwa wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili kutunza thamani na kukuza uchumi wa maeneo yao kwa muda mrefu zaidi.

Mchengerwa kando ya kusisitiza weledi na kasi katika kutekeleza miradi hiyo jijini Arusha, amepongeza waratibu wa Mradi wa TACTIC kwa kutoa tenda ya ujenzi wa miundombinu hiyo kwa Mkandarasi mzawa, akisisitiza kuwa kutumika kwa wakandarasi wazawa kunakuza mzunguko wa fedha na kutoa ajira zaidi kwa wazawa tofauti na ambavyo angetumika Mkandarasi wa kigeni katika utekelezaji wake.

Kadhalika Waziri Mchengerwa ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya TACTIC katika maeneo yao akiwakumbusha kuwa maendeleo yanayofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan si zawadi bali ni wajibu wa waliopata bahati kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan akiwataka kusimamia wajibu wao kikamilifu katika kufanikisha malengo na mipango mbalimbali iliyokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *