Mchechu aeleza mapinduzi Sheria Uwekezaji wa Umma

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam
MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma utaleta mapinduzi makubwa katika taasisi za umma kwa maendeleo yenye tija.
Muswada huo uliosomwa bungeni jijini Dodoma kwa mara ya kwanza Novemba 10, 2023, umelenga kuweka masharti ya uwekezaji wa umma.
Pia kuweka mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu wa usimamizi wa uwekezaji wa umma, usimamizi wa mashirika umma na kufuta sheria ya mamlaka na majukumu ya Msajili wa Hazina nchini (TR).
Mchechu aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Mamlaka hiyo itafanya mapitio ya utendaji wa kifedha wa mashitika ya umma ili kubaini mahitaji na kupendekeza kwa kamati njia bora za uwekezaji wa kifedha.
Kuweka vigezo vya mashirika ya umma kupata fedha za uwekezaji, kuidhinisha maombi ya shirika juu ya kununua hisa, kuwekeza au kuonosha uwekezaji katika mashirika ya umma na maeneo mengine yenye fursa kibiashara.
Pia kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha michango na gawio kutoka mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali inamiliki hisa vinalipwa kwa wakati.
Kufuatilia utendaji wa mashirika ya umma kwa lengo la kutathmini uendelevu wake na kupendekeza hatua stahiki ikiwemo kuunganisha, kufuta mashirika husika au kuboresha utendaji kazi wake.
Mchechu alisema, Muswada huo utatoa fursa ya kuanzishwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ambao utawezesha upatikanaji wa mitaji kwa haraka.
Mfuko huo utaainisha vyanzo vya fedha ambavyo ni pamoja na maduhuli yatakayokusanywa na mamlaka, kiwango chake kitabainishwa katika kanuni.
Pia mfuko huo utakuwa chini ya uangalizi wa kamati ya uongozi ya mfuko, kuwa na miongozi ambayo itaainisha vigezo vya uwekezaji, ufuatiliaji na mambo mengine yanayohusu uendeshaji wa mfuko.
Msechu alisema, faida za mfuko huyo ni pamoja na serikali kufanya uwekezaji wa kimkakati kwa wakati, kuongeza ufanisi wa uendeshaji.
Pia kuokoa mashirika ambayo bila mfuko huo yanaweza kuanguka pamoja na kuwezesha mashirika ya umma kustahimili ushindani.
Katika hatua nyingine, Mchechu alisema Serikali ya Tanzania imefanya uwekezaji wa sh. trillioni 73 katika taasisi, mashirika ya umma na Wakala wa Serikali 298 zinazofanya shughuli mbalimbali, asilimia 86 za taasisi hizo zikitoa huduma za kijamii.
Alisema kutokana na mikakati iliyopo, baada ya miaka mitano, baadhi mashariki yanakwenda kufanya vizuri, watendaji wa mashirika hayo watapimwakwa ufanisi wa kazi ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa.
“Mwaka 2021/2022 mashirika 136 yameweza kupata mapato ya sh. bilioni 645, mwaka 2020/2021 mashirika 200 yalipata sh. bilioni 477, mwaka 2019/2020 mashirika 236 yameingiza mapato ya sh. bilioni 696.
“Umefika wakati wa Wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi wa uweledi ili kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.
“Ili mashirika ya umma yapige hatua yanapaswa kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake, kuwekeza rasilimali fedha ili kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo.
“Pia kuwekezana malengo na wasimamizi ili kufikia viwango vya mafanikio ndani ya muda Fulani,” alisema.
Aliongeza kuwa, mipango iliyopo ni kuweka utaratibu wa kuishirikisha Mamlaka kwenye mchakato wa kuwapata wenyeviti, wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi jambo ambalo litasaidia ufanisi wa kazi.
Alifafanua kuwa, mashirika na taasisi za umma zinapaswa kuwekewa mifumo rafiki ambayo itasaidia kutengeneza mapato na kuleta tija kwa Taifa.
“Ili kufikia malengo, tumependekeza mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (PIA) kwa kubadilisha jina la Ofisi ya Msajili kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority-PIA),” ALISEMA.
Lengo ni kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji uchumi wa duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *