Mbio za Mbuzi kutimua vumbi Sept. 21, 2024

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TAMASHA la mbio za Mbuzi lililoandaliwa na Klabu ya Rotary Oysterbay, linatarajia kufanyika Septemba 21, mwaka huu, kwa lengo la kukusanya Sh. milioni 400 za kusomesha wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Rais wa Klabu ya Rotary Oysterbay, Himanshu Bhattbhatt, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha hilo.

Amesema tamasha hilo linalotarajia kuhusisha washiriki 4,000, litafanyika kwa mara ya saba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018, kwa lengo la kushirikiana na serikali kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Mbio za Mbuzi mwaka huu zitafanyika Septemba 21 na leo tupo hapa kutangaza wadhamini wetu walikitokeza kutuunga mkono kufanikisha mbio hizi zenye lengo la kusaidia jamii moja kwa moja,” amesema.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika  katika Viwanja vya The Green Oysterbay jijini Dar es Salaam kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 2:00 usiku.

Amesema kupitia tamasha hilo, washiriki ambao ni watu wazima na watoto watapata burudani mbalimbali kupitia michezo iliyoandaliwa na washindi watapatiwa zawadi mbalimbali.

Naye Mratibu wa mbio hizo kwa mwaka huu, Paul Muhato alisema, “Tuna furaha kuwa na Vodacom Tanzania kama mdhamini mkuu na tunawashukuru wadhamini wetu ambao wengi wao wanajiunga nasi kwa mara nyingine tena kwa kuendelea kutuamini na kuungana na sisi katika kuandaa mbio hizi. 

“Tuna imani kwamba Mbio za Mbuzi za mwaka 2024 zitakuwa zitakuwa kielelezo cha nguvu ya ushirikiano katika kuchangia maendeleo ya elimu Tanzania. Washiriki wajiandae kupata kilicho bora kutoka kwa timu yetu, watoa huduma na wauzaji wa bidhaa mbalimbali. Katika maandalizi ya mwaka huu tunashirikiana na wanachama, marafiki na wanafamilia wa Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay, washirika wetu, wauza chakula na vinywaji, serikali ya mtaa na wadau wengineo wengi,” amesema.

Paul ameendelea kwa kueleza kuwa, tiketi ya kawaida kwa mtu mzima ni Sh. 30,000 na watoto Sh. 10,000, huku VIP zikipatikana kwa kati ya Sh. 200,000 -250,000 na Sh. 30,000 kwa watoto.

Mbio za mwaka huu zinaandaliwa kwa udhamini wa mashirika mbalimbali ikiwamo Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wakuu, EATV, Tanzanite Dreams, YARA, Toyota, Pepsi, GardaWorld, Abstrat PR & Marketing, RedNWhite, TBL, Trellidor, JC Decaux, Slipway, Bowmans Law, Oryx. Energies, Pesapal, Le Grande Casino, Bobo, Premier Care, Jibu, na Minet.

Kampuni hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha mbio za mwaka huu zinafana kupitia mchango wa fedha taslimu na huduma au bidhaa.

Mwakilishi wa EATV, Mariam Shabani, amesema wameguswa kudhamini mashindano hayo kwa sababu yanagusa jamii moja kwa moja.

Naye Mkuu wa Uhusiano kwa Umma na vyombo vya habari wa Vodacom, Annette Kanora, amesema wamevutiwa kuendelea kuwa wadhamini kwasababu wameshuhudia jamii ikinufaika.

“Baada ya kuona mafanikio yaliyotokana na mbio za mbuzi za mwaka 2023, kampuni imevutiwa kuendelea kudhamini mbio hizi za hisani kwa mwaka wa pili mfululizo,” amesema Annette.

Mwakilishi wa Kampuni ya The Tanzanite Dreems inayojihusisha na vito vya thamani, Shadya Latiff, amesema wanaona kuna haja ya kugusa jamii yenye uhitaji hususani sekta ya elimu.

Mbio za mwaka jana zilikusanya Sh. milioni 340 ambazo zilitumika kusaidia wanafunzi wa vyuo vikuu wenye uhitaji katika kufanikisha malengo yao ya kupata elimu.

Fedha hizo zinatumika uboresha mazingira ya elimu, kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji na kuimarisha miundombinu ya maji na usafi shuleni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *