Mbinga yahamasisha chanjo ya kuku

Na Stephano Mango, Mbinga 

WAFUGAJI wa kuku  Halmashauri  ya Wilaya ya Mbinga, wamekumbushwa kuchanja mifugo hiyo ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali na kupunguza gharama za matibabu pindi  wanakapougua.

Wito huo umetolewa jana na Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Haruna Masige,  alipozungumza katika kipindi cha radio ‘Mbinga Yetu’ kinachorushwa na Radio Hekima.

Masige amesema kuwa kuanzia siku ya kwanza kifaranga  anapototolewa kinatakiwa kipate chanjo, katika umri huu wa siku moja kifaranga huwa kinashambuliwa na ugonjwa unaitwa Mahepe.

Ameendelea kueleza kuwa, katika siku ya 7 kuku anatakiwa apate chanjo ya ugonjwa wa Gumboro  ambayo itarudiwa tena siku ya 21.

Siku ya 14 kuku anatakiwa apate chanjo ya ugonjwa wa Mdondo maarufu kama Kideri ambayo itarudiwa tena siku ya 30, kuku akiwa na umri wa miezi miwili hupewa chanjo ya ndui.

Pamoja na  hayo Masige amewakumbusha wafugaji  kuzingatia usafi katika banda  la kufugia  kuku na mazingira yake pamoja na  usafi wa vyombo  vya kulishia ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa.

Amewataka wafugaji kuendelea kupata elimu na taarifa mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ili waweze kukusaidia kufuga kwa tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *