WARSAWA, Poland
MSHAMBULIAJI Kylian Mbappe, ameanza vyema maisha yake ya soka ndani ya Real Madrid baada ya kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza na kuiwezesha timu yake kushinda taji la Super Cup kwa kuifunga Atalanta kwa jumla ya mabao 2-0.
Mchezo huo wa fainali ambao uliwakutanisha kati ya bingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na bingwa wa michuano ya Ligi ya Europa ulichezwa katika uwanja wa Taifa wa nchini hapa uliopo katika Mji wa Warsaw.
Miamba hao walishindwa kufungana hadi filimbi ya mapumziko inapulizwa lakini dakika ya 58 kipindi cha pili, Federico Valverde alisukumiza mpira wavuni akimalizia kazi nzuri kutoka kwa winga Vinicius Jr.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha zaidi Madrid ambapo dakika 10 mbele, kiungo Jude Bellingham alimmegea pasi safi ya ndani ya boksi, Mbappe ambaye bila ajizi aliukwamisha mpira huo wavuni na kuihakikishia timu yake ubingwa wa kwanza msimu huu.
Hilo linakuwa ni taji la kwanza kwa Mbappe ambaye amejiunga na Madrid kwenye majira haya ya kiangazi akitokea PSG ya Ufaransa kwa uhamisho huru.
Ubingwa huo pia unamfanya Kocha, Carlo Ancelotti kufikisha idadi ya mataji 14 akishinda na Madrid kwa vipindi viwili tofauti alivyohudumu ndani ya miamba hao.