Mavunde awakaribisha nchini wawekezaji wa madini kutoka Finland

-Finland yaahidi kushiriki kwenye utafiti wa madini

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewakaribisha jumuiya ya wa Wafanyabiashara kutoka nchini Finland, kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali ya kutosha ya madini, mazingira ya uwekezaji rafiki na sera zinazotabirika.

Waziri Mavunde ameyasema hayo jana Masaki Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kifungua kinywa ulioandaliwa na Ubalozi wa Finland nchini, kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wa Madini kutoka Finland na Wizara ya Madini ili kubaini maeneo ya ushirikiano na fursa za kiuchumi zilizopo sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting, amesema Tanzania na Finland ni nchi zenye ushirikiano mkubwa kwenye masuala ya kiuchumi na hivyo ni wakati muafaka kuimarisha uhusiano kupitia uwekezaji kwenye sekta ya madini.

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukuza sekta ya madini nchini na kuifanya kuwa muhimu kwenye kuchangia maendeleo ya uchumi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini ya Finland (GTK) Prof. Tiilikainen Kimmo alisema kwamba kupitia makubaliano (MoU) kati ya GTK na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini(GST),Finland itashirikiana na serikali kuimarisha shughuli za Utafiti wa madini ili kuiwezesha Tanzania kufikia Dira ya 2030 ya Madini MAISHA na UTAJIRI ambapo Tanzania imejipanga kufanya utafiti wa kina wa madini wa kufikia eneo la asilmia 50 la eneo la nchi nzima.

Akiwasilisha hotuba yake Waziri Mvunde, aliwakaribisha wafanyabiashara kutoka Finland kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kiuchumi kupitia sekta ya madini na hasa madini mkakati ambayo kwa sasa yana uhitaji mkubwa duniani.

“Rais Samia kupitia falsafa yake ya uongozi wa 4R ameweka mazingira rafiki ya biashara na uwezekaji nchini Tanzania na hivyo Tanzania ni sehemu salama ya kufanya uwekezaji.

Tanzania imejaaliwa rasilimali madini ya kutosha na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa na nafasi nzuri kuvutia uwekezaji. Hivyo tunafungua milango kwa wafanyabiashara kutoka nchini Finland kuchangamkia fursa za uwekezaji kupitia sekta ya madini,” alisema Mavunde

Wafanyabiashara hao wapo nchini kuhudhuria mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji 2024 unaofanyika nchini ambao umefanyika kwa siku tatu na unamalizika leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *