Tatu Mohamed, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema kuwa mauzo ya umeme nchini yameongezeka kutoka Trilioni 1.6 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Trilioni 1.8 mwaka 2021/22.
Hayo yamebainishwa Julai 27, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Fedha Tanesco, Renata Ndege wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya Tanesco, Msajili wa Hazina na wahariri wa vyombo vya habari.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022 shirika hilo limeongeza mauzo ya umeme kwa asilimia 11 na faida kwa asilimia 42 ukilinganisha na kipindi cha mwaka jana.
“Gharama za uzalishaji na matengenezo nazo zimeongezeka kutoka Trilioni 1.5 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Trilioni 1.6 mwaka 2021/2022,” amesema Ndege.
Hata hivyo amesema kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2022 shirika hilo limefanikiwa kupata kiasi cha Sh. Trilioni 2.5 kwa ajili ya mradi ya kimkakati ya ufuaji umeme, uzalishaji na usambazaji.
Amesema fedha hizo zimepokelewa kutoka serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo wakiwemo Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Korea (EDCF), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Ufaransa na Shirika la Maendele la Ujerumani (KFW).
Amesema hivi sasa shirika hilo halitengenezi tena hasara bali limekuwa shirika linalotengeneza faida.
Ameongeza kuwa, hali ya fedha inaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka, ambapoi mwaka jana tumepata faida Sh bilioni 109.4 kutoka Sh bilioni 77 za mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande, amesema utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme katika Bwawa la Julius Nyerere umefikia asilimia 90 na kwamba Juni 2024 watawasha umeme.
“Mradi huu ni muhimu kwa sababu unagharimu Dola zaidi ya bilioni 3.5 na umeme huu ukipatikana utatosheleza mahitaji hata zikiungwa nyumba zote Tanzania,” amesema Chande.