Mashindano ya NMB ‘Interzone League 2024’ yafana Mwanza

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuhakikisha wafanyakazi wake hapa nchini wanakuwa na afya njema ili waweze kutoa huduma bora kwa wateja wao, Benki ya NMB, imefanya mashindano maalum ya kikanda kwa matawi yao upande wa michezo ya soka na netiboli ‘pete’.

Mashindano hayo yalijulikana kwa jina la ‘NMB Interzone League 2024’ ambayo yalifanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa kushirikisha zaidi ya wafanyakazi 500 kutoka matawi zaidi ya 200 ya benki hiyo.

Yalikuwa ni mashindano ya kipekee kwani yalitoa mwitikio chanya kwa wafanyakazi kujenga umoja, ushirikiano, kufahamiana, hamasa na kuimarisha afya kwa kufanya mazoezi.

Michezo hiyo ilianza katika ngazi ya kanda na fainali zake kuhitimishwa Desemba 4, mwaka huu katika uwanja huo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tano kulia), akiongoza mazoezi ya viungo kujenga afya kabla ya kuanza kwa mashindano ya NMB Interzone League 2024 ambayo yalifanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Kushoto kwake ni Mhazini wa benki hiyo, Aziz Chacha na kulia kwake ni Meneja wa Kanda ya Ziwa wa NMB, Faraja Ng’ingo.

Wafanyakazi hao walianza kwa mazoezi ya viungo kujenga afya, kujengewa uwezo wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kufanya vipimo na ushauri na kuchangia damu.

Fainali hizo zilitanguliwa na Tamasha la Wellness Day lililobebwa na kaulimbiu ya ‘Your Health is our priority’ likilenga kuimarisha afya za wafanyakazi wake na utendaji kazi wao kupitia michezo ikiwa ni mwendelezo wa kuhakikisha inaendelea taasisi kinara inayotoa huduma bora na yenye wafanyakazi imara.

Katika mchezo wa utangulizi ulioanza saa 6:56 mchana, iliikutanisha timu ya mameneja mashabiki wa Yanga dhidi ya mameneja wa Simba ambapo katika mchezo huo, Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Joel Uswege dakika ya 25 na Revocatus Rulazya dakika ya 57, huku bao la Simba likipachikwa na Grayson Komba dakika ya 14.

Kwa upande wa fainali mchezo wa netiboli uliochezwa saa 9 alasiri, timu ya Kanda ya Kati ‘Central Zone’, iliibuka mabingwa wa mchezo huo kwa kuitandika Highland Zone magoli 42-22.

Katika mashindano hayo, mechi ya mwisho ambayo ilihitimisha tamasha hilo ilikuwa kati ya Kanda ya Kaskazini ‘Northern Zone’ na Kanda ya Magharibi ‘West Zone’ katika fainali ya mchezo wa soka iliyopigwa kuanzia saa 10:30 jioni Uwanja wa CCM Kirumba huku Northern Zone ikienda mapumziko kifua mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Simon Zuberi.

West Zone ilisawazisha bao hilo kipindi cha pili dakika ya 47 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Alex Mwaisaka na kufanya mambo kuwa magumu hadi dakika ya 90 za mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, huku Northern Zone wakiibuka mabingwa kwa ushindi wa penalti 5-4, ambapo mchezaji Hamis Said wa Northern Zone aliichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Washindi hao walikabidhiwa zawadi mbalimbali ambapo bingwa wa soka ambaye ni Northern Zone, ilipewa sh. milioni 2, kombe na medali, mshindi wa pili ambayo ni West Zone iliambulia sh. milioni 1 na medali, huku bingwa wa Netiboli, timu ya Central Zone ikipata sh. milioni 1.5, kombe na medali na mshindi wa pili, timu ya Highland Zone ikipata sh. 750,000 na medali.

Wachezaji wa netiboli wakichuana

Kwa mujibu wa Mkuu Idara ya Rasirimali Watu Kanda NMB Makao Makuu, Lameck Kehanga, amesema mashindano hayo yamelenga kuimarisha afya, kudumisha ukaribu baina yao na kuendeleza utaratibu wao wa kujenga afya kupitia mazoezi kwani wanatambua afya ndiyo mtaji na ubora wa afya ndiyo ubora wa taasisi kwani wafanyakazi wenye afya ndiyo watazalisha kwa ubora na uendelevu.

Kehanga ambaye pia ni Mratibu wa mashindano hayo, amesema wana imani kubwa huduma za wateja zitaimarika kupitia mashindano hayo na NMB kuendelea kuwa kinara kwenye uzalishaji kwa sababu wanajenga nguvu ya wafanyakazi wenye afya iliyo njema ambao wataendelea kuhakikisha malengo ya kampuni hiyo yanasonga mbele kila siku.

“Tunajua michezo ni furaha kwa kupitia mashindano haya tuna imani kubwa hata furaha za wafanyakazi wetu zimeongezeka na furaha zikiongezeka maana yake wafanyakazi watatoa pia hiyo furaha kwa wateja wetu wanapokwenda kupata huduma zetu kwenye matawi yetu,” amesema Kehanga.

Ameongeza: “Tumekuwa na wataalam kutoka taasisi mbalimbali ambao wametupima kujua hali zetu za kiafya na kutushauri namna bora ya kuishi ili tuendelee kuboresha afya zetu na wametueleza mambo mengi namna gani tunavyoweza kuyazingatia ili tuendelee kuwa na afya bora kwa ajili ya kampuni na kwa ajili yetu binafsi.”

Amesema tamasha hilo lina faida nyingi ikiwemo kusaidia wafanyakazi kuimarisha afya, kuwaleta pamoja wafanyakazi na kuwa wamoja na kufahamiana, kutengeneza mtandao namna gani wanavyoweza kuipeleka benki hiyo kwa pamoja na kujenga timu yenye lengo moja.

Kwa upande wa Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Upimaji wa Afya kwa Jamii kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Pedro Pallangyo, amesema walitoa huduma za upimaji wa kibingwa za moyo ikiwemo mashine kubwa ya kupima utendaji kazi wa moyo, kutambua kama moyo una ugonjwa wa aina yoyote, na kutoa elimu kwa wafanyakazi wa NMB kuhusu sababu hatarishi na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Ili wazalishe na kutimiza majukumu yao kama wafanyakazi wa NMB lazima wawe na afya bora na moyo ni kiungo muhimu katika utendaji kazi wa mwili wa mwanadamu na kumpa nguvu ya kutimiza majukumu yake ndiyo maana tunawaeleza wahakikishe mioyo yao inabaki katika afya bora ili majukumu ya kazi yafanyike kwa ufanisi mkubwa,” amesema Dkt. Pallangyo.

Pia Munasihi kutoka Damu Salama Kanda ya Ziwa, Florence Masamu ambao walishiriki katika Wellness Day ya NMB, ameipongeza benki hiyo kwa kuwapa fursa wafanyakazi wake kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania wenye uhitaji huku wakikusanya chupa 150 za damu katika zoezi hilo.

“Ni jambo zuri lililofanywa na watumishi hawa wa NMB kwa sababu wanasaidia jamii kwa kuokoa wenzetu wenye mahitaji ya damu. Kuna faida nyingi kwao wanapochangia damu kwa sababu inaimarisha afya kwa kupunguza shinikizo la damu, kuimarisha misuli na kumfanya mtu kuwa vizuri katika hali ya kiafya,” amesema Florence.

Nahodha wa mabingwa wa soka, Northern Zone, David Sida, ameipongeza taasisi hiyo kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yameleta msisimko kwa wafanyakazi huku akiiomba kuyafanya yawe na mwendelezo kwani yamekuwa na motisha kwao na yameleta ufanisi katika utendaji kazi.

“Mashindano yalikuwa mazuri tunashukuru uongozi wa NMB kwa kuyaandaa na viongozi wetu wa kanda kwa kutuunga mkono haikuwa rahisi kuwa mabingwa jitihada na jasho tulilopambana imetulipa kwa sababu mashindano yalikuwa magumu kila timu ilijipanga ndiyo maana fainali imekuwa ngumu,” amesema Sida.

Kwa upande wa Nahodha wa mabingwa wa Netiboli Central Zone, Sammy Lema, amesema:“Tumepokea ushindi huu kwa furaha, jasho letu limeleta matunda huu ni mwanzo tu kwa sababu ushindi huu umetupa chachu tutakwenda kujipanga zaidi kwa ajili ya mwakani.

Washindi wa netiboli wa michuano ya NMB Interzone League kutoka Central Zone, wakishangilia na kombe lao baada ya kuibuka mabingwa wa mashindano hayo.

“Mashindano haya yametuunganisha na kufahamiana kwahiyo yana faida kubwa tumekuwa na ushirikiano wa kiakili, utendaji kazi na kusukuma zaidi gurudumu la NMB.”

Kwa upande wa Meneja wa Tawi la  NMB Mazengo, Victor Dilunga ,ambaye alikuwa nahodha wa timu ya mashabiki wa Simba, amesema michezo hiyo ni mizuri kwani inadumisha afya zao na akili, urafiki, kufahamiana na kujenga umoja kwani wanapocheza pamoja wanadumisha undugu na urafiki na kuimarisha afya zao kwa ajili ya kazi na kulitumikia taifa.

“Katika tukio hili kama wafanyakazi tumenufaika na vitu vingi tumepima afya zetu, tumechangia damu kwa ajili ya watanzania wenzetu wenye uhitaji tunajisikia faraja kuchangia uhai wa watu wengine lakini kwa ujumla na kujua afya zetu tunapokuwa kwenye matamasha kama haya,” amesema Dilunga.

Kwa upande wake, Nahodha wa Mashabiki wa Yanga, Abraham Mbise amesema: “Tunashukuru Mungu kwa ushindi na tunawapa pole wenzetu wa Simba, mashindano haya yanatujenga kiakili na yanatusaidia katika kuweka miili yetu fiti kwa ajili ya kazi na kuimarisha utendaji kazi wetu, hivyo, ushindi huu ni motisha na hamasa kwetu kuendelea kujiweka fiti na kuwa tayari muda wote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *