Marekani yaibuka bingwa wa jumla Olimpiki

PARIS, Ufaransa

TAIFA la Marekani, limeibuka mbabe wa jumla wa michuano ya Olimpiki nchini Ufaransa baada ya kushinda medali 40 za dhahabu sawa na China.

Hata hivyo Marekani wao ilishinda pia jumla ya medali 44 za fedha na 42 za shaba na kufanya jumla ya medali 126 tofauti na China ambao wana jumla ya medali 91 baada ya pia kushinda fedha 27 na shaba 24.

Medali ya 40 ya dhahabu ya Marekani, imepatikana siku ya mwisho ya kufunga mashindano Jumapili ambapo timu yao ya mpira wa kikapu ya wanawake iliibuka na ushindi wa vikapu 67-66 dhidi ya wenyeji Ufaransa.

Hii ni mara ya nne mfululizo katika mashindano ya Olimpiki, Marekani kuibuka kinara katika upande wa kukusanya medali.

Wenyeji timu ya Taifa ya Ufaransa, wamemaliza nafasi ya tano katika msimamo wa medali wakiwa wamenyakuwa 64. Katika medali hizo, 16 ni dhahabu, 26 ni fedha na 22 ni shaba.

Barani Afrika, Kenya imeibuka vinara wakishika nafasi ya 17 baada ya kushinda jumla ya medali 11. Katika hizo 4 ni dhahabu, 2 fedha na 5 ni shaba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *