Maono ya Samia kwenye mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu

Na Daniel Mbega
MIEZI michache baada ya kushika hatamu za uongozi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ameonyesha dhahiri alivyodhamiria kuendelea kuitekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hasa katika kuleta mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu.
Japokuwa Ilani hii iliandaliwa wakati wa Awamu ya Tano, lakini ni wazi utekelezaji wake umeanza katika Awamu ya Sita chini ya Mama Samia, mwanamke wa shoka mwenye maono mapana ya kiuchumi, huku akikazia pia kuwainua wanawake, siyo katika uchumi pekee, bali hata katika nafasi za uongozi.
Nilibahatika kuzipitia ilani za uchaguzi za vyama vitatu vya CCM, ACT na Chadema hata kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na ni CCM pekee ambayo Ilani yake ya mwaka 2020-2025 imeeleza kinagaubaga katika Sura ya Pili kuhusu “Mapinduzi ya Uchumi kwa Maendeleo ya Watu”.
Ikumbukwe kwamba, Ilani (Manifesto) ni tangazo linalozungumzia masuala ya kimaendeleo ambayo endapo chama kitachaguliwa, kushinda uchaguzi na kuunda Serikali basi mambo hayo yatatumika kutengeneza mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu.
Sura hii ya pili imesheheni kurasa 115, kuanzia Ukurasa wa 9 hadi 124, huku maelezo ya uchambuzi wao kuhusu maendeleo ya watu ukiwa umewekwa katika aya zenye nambari, jambo ambalo linawezesha usomaji wa rejea na wenye mtiririko unaoeleweka.
Katika aya ya 12, CCM wanasema wanaendelea kutambua umuhimu wa kujenga uchumi wa kitaifa ili kuhakikisha kwamba Watanzania ndio wanufaika wakuu wa uchumi na maliasili za nchi.
Katika muktadha huo, CCM kwenye ilani yake ili iweze kujenga uchumi wa kunufaisha Watanzania, wamejikita katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda na uchumi fungamanishi, jumuishi na shindani unaotumia sayansi na teknolojia za kisasa na ambao unahimili utandawazi na unaoweza kutumia kikamilifu fursa zake kwa kuuza zaidi bidhaa za viwandani na bidhaa nyingine nje ya nchi.
Kwa mantiki hii CCM wanaamini kuwa ili kuleta maendeleo kwa watu hapuna budi kuendeleza viwanda, kukuza uzalishaji wa kisasa kabisa, kuongeza ajira na hatimaye kuuza bidhaa kwenye masoko ya ushindani ndani nje ya nchi, jambo ambalo Rais Samia analifanya kwa dhati.
Katika aya ya 14, CCM inasema inathamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kujenga uchumi wa kitaifa na wenye ushindani, huku wakionelea kuwa ni vema sekta binafsi ikajikita kwenye uzalishaji wa bidhaa za viwandani hususan katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii na sekta nyingine zote.
CCM imetoa ahadi kubwa kwa sekta binafsi na inaendelea kutekeleza ahadi hiyo ya kampeni na Ilani ya Uchaguzi. Wao wamesema kuwa, na nitanukuu; “CCM itaendelea kusimamia serikali zake kuhakikisha sekta binafsi inalindwa na kuendelezwa na kwamba haki ya kila mtu, kikundi, ushirika na kampuni ya kuendesha shughuli za uchumi na biashara kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria zinalindwa wakati wote.
“Masuala mawili ambayo CCM itasimamia kwenye sekta binafsi kama ilivyoahidi ni uhuru wa watu kufanya shughuli za kiuchumi na biashara lakini pia kwa kufuata sheria”.
Katika aya ya 17 (x), CCM imeiahidi sekta binafsi na Watanzania wafanyabiashara kuwa itajikita kwenye kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment) kwa kutatua changamoto zinazokabili uwekezaji na ufanyaji biashara.
Ndiyo maana Rais Samia, hata alipokuwa katika Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, aliwahamasisha wawekezaji kutoka nje waje wawekeze katika sekta zote, kwani mazingira ni rafiki.
Sina mashaka pia hili litafanywa na Mabalozi wetu wanaotuwakilisha katika mataifa mengine, na hata alipowaapisha mabalozi wanne hivi karibuni, Rais Samia aliwahimiza kujali uzalendo.
Ili kufanikisha haya yote, Ilani ya CCM inasema ipo misingi mikubwa mitano, ambayo itasimamisha nguzo za ujuzi wa mapinduzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Misingi hiyo imetajwa kwenye aya ya 14 kuwa ni uwepo wa amani na usalama, utawala wa sheria na utulivu wa kisiasa, mwenendo tulivu wa uchumi mpana (macroeconomic stability); ubora wa miundombinu na huduma wezeshi kama vile uchukuzi, nishati na mawasiliano; urahisi, ufanisi na uhakika wa sheria, kanuni, taratibu na utendaji wa sekta ya umma katika kuwezesha shughuli za uchumi na biashara za sekta binafsi na uwepo wa rasilimali watu ya kutosha yenye elimu, ujuzi na maarifa stahiki hususan katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Ilani hiyo pia kwenye aya yake ya 15, inasema kuna sekta za uchumi na biashara ambazo endapo sekta binafsi itashindwa kuwekeza basi Serikali ya CCM itaweza “kujihusisha moja kwa moja kwenye shughuli za uchumi na biashara za kimkakati na zile ambazo sekta binafsi haijaweza kujihusisha nazo kwa ufanisi au haivutiwi kuwekeza.”
Ni katika sura hii ya pili ambapo Ilani ya CCM imechambua viashiria mbalimbali vya uchumi kwa kuelezea hali ya uchumi wa nchi ilivyo. Viashiria vya uchumi vilivyobainishwa ni ukuaji wa Pato la Taifa kwa asilimia 6.9 kati ya mwaka 2016 na 2019, pato la wastani kwa kila mtu kutoka milioni 1.9 (Dola za Marekani 992) mwaka 2015 mpaka kufikia Dola za Marekani 1,086 sawa na Shs. milioni 2.4 mwaka 2018.
Hilo ni sawa na ongezeko la dola 94 kwa miaka mitatu yote tangu 2015 mpaka 2018 na ni sawa na ongezeko la dola 31.3 kwa mwaka.
Kwa fedha za Kitanzania ongezeko hilo la pato la wastani kwa kila mtu ni sawa na ongezeko la Shs. 489,531 kwa miaka mitatu na Shs. 163,177 kila mwaka, na kwa kiasi kikubwa ndilo limefanya mwaka 2020 Tanzania ikatangazwa kuwa nchi ya uchumi wa kati wa chini kabla hata ya kufikia mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuelekea mwaka 2025.
Wastani wa miaka ya kuishi kuongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 mpaka miaka 65 mwaka 2020, usambazaji wa umeme vijijini kuongezea kutoka asilimia 16.4 mwaka 2015 mpaka asilimia 67.1 mwaka 2019.
Kwenye Ilani hii, CCM wanahitimisha kutaja viashiria vya uchumi kwa kuzungumzia hali ya umaskini wakisema kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 mpaka asilimia 26.4 mwaka 2017/18, pia wakisema kuwa umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 mpaka asilimia 8.0 mwaka 2017/18.
Takwimu hizo za umaskini pamoja na kuvutia kwake bado siyo takwimu za siku za hivi karibuni kama mwaka 2019 au 2020.
Aya ya 23 ya Ilani ya CCM inazungumzia masuala ya kupambana na umaskini na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Katika aya hiyo CCM imesema kuwa, tayari ilifanya miradi takriban kumi ya ujasiriamali kwa ajili ya vyama vya ushirikia kwenye kilimo, upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiriamali wanawake zaidi ya 3,000 nchi nzima kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara, halmashauri 185 kutoa mikopo yenye thamani ya Shs. 93.3 bilioni katika Mfuko wa Kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu huku wanufaika wakiwa takriban vikundi vya wajasiriamali 32,553.
Ni katika aya ya 26 CCM imetoa ahadi 14 kwa ajili kuendeleza miradi ya kuwezesha wananchi kiuchumi.
Aya ya 27 wamezungumzia masuala watakayofanya kwenye uchumi wa rasilimali za maji (Blue Economy) na aya ya 28 ilani hiyo imezungumzia ahadi za kutumia fursa za kijiografia za nchi yetu kuchochea maendeleo.
Katika aya ya 32, CCM wameachambua jinsi watakavyoongeza fursa za ajira milioni 7 kupitia ahadi 19 za fursa kwenye halmashauri, uwekezaji kwenye misitu, programu za kujitolea, atamizi za ubunifu, mifuko ya hifadhi ya jamii, SACCOSS na makampuni.
Haya ndiyo yanayotekelezwa na Serikali ya Mama Samia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *