Na Mwandishi Wetu
Kisarawe
TAKRIBAN watendaji wa vijiji 24 kati ya 66 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani hawana ajira za kudumu kwa miaka sita sasa.
Kati ya watendaji hao, wawili walishafariki wakiwa kazini na mmoja aliamua kuacha kazi kutokana na kulipwa posho yake kwa miezi takriban sita mfululizo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba, watendaji hao waliajiriwa mwaka 2017 kwa kutumia utaratibu wa ‘Kazi za muda mfupi’ katika jitihada za Serikali kukabiliana na uhaba wa watumishi wa umma.
Kulingana na uchunguzi huo, wafanyakazi hao walipewa mikataba ya kipindi cha miezi mitatu kwa utaratibu kwamba kila baada ya muda huo wangekuwa wanasainishwa mkataba mpya jambo ambalo linadaiwa kufanyika, lakini taarifa zinaonyesha kwamba, kwa zaidi ya miezi sita sasa hawajapewa mkataba mwingine.
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe yenye jumla ya watu 108,398 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ina jumla ya tarafa nne (Cholesamvula, Maneromango, Mzenga na Sungwi), vijiji 66 na vitongoji 235. Ni miongoni mwa halmashauri tisa za mkoa wa Pwani ambapo ilianzishwa tangu Julai Mosi, 1907.
Gazeti hili limebaini kwamba, watumishi hao wamekuwa wakiishi hata kwa zaidi ya miezi sita bila posho ambapo hadi gazeti hili linakwenda mitamboni jana, inaelezwa kwamba walikuwa wanadai posho za miezi takriban kumi ambazo hawajui lini watalipwa.
Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba, wakati mwajiri wao anapoamua kuwalipa, mara nyingi hulipa posho ya mwezi mmoja tu na mingine iliyosalia huambiwa kwamba watalipwa hali ya fedha itakapokaa sawa, jambo ambalo huwa halitekelezwi.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baadhi ya watendaji walioajiriwa wakati huo ambao majina yao tunayahifadhi walipangwa katika vijiji vya Kikwete, Maneromango Sokoni, Maneromango Kaskazini, Malui, Bomani Kisarawe, Malangalanga, Ngongele Kidugaro.
Wengine walipangwa vijiji vya Kului – Mzenga, Mlowo – Kibuta, Sanze Kisarawe, Sungwi, Mafumba – Cholesamvula, Mwanzo Mgumu na Msimbu wilayani humo.
Watendaji hao wa vijiji wanaojitolea (vibarua) hawana likizo yoyote kwa miaka yote sita na wala hawapati haki nyingine za msingi za kikanuni kama zinavyotajwa na Kanuni za Utumishi wa Umma kwa wale walio na ajira ya kudumu.
Wachunguzi wa masuala ya utawala wanaeleza kwamba, kutokuwapa ajira za kudumu watendaji hao kwa miaka yote sita ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, lakini pia ni uvunjaji wa sheria za ajira, zikiwemo za kimataifa.
“Hivi katika kipindi cha miaka sita Serikali haijatoa hata ajira chache tu kwa Tamisemi? Kwa nini basi ajira hizo wasipewe wale ambao tayari wako kwenye utumishi wa muda na badala yake waajiri wengine wapya?” anahoji Mohammed Athumani Pazi, mkazi wa Maneromango.
Javan Sylvester, mkazi wa Kazimzumbwi wilayani humo, anasema kutokuwapa ajira za kudumu (kutowathibitisha kazini0 watumishi hao kunatengeneza mianya ya rushwa hasa ikizingatiwa kwamba, japokuwa wao wanajitolea, lakini ndio wasimamizi wakuu wa shughuli za Serikali na wanakusanya mapato.
“Mtendaji analipwa posho kiduchu, anakaa miezi sita, saba hajapata hata hiyo posho, lakini anawajibika kukusanya mapato ya kijiji na kusimamia miradi mingine, hivi kwa mazingira hayo hawezi kushawishika kudokoa fedha ili walau watoto wake wapate kula?” anahoji Javan, na kuongeza;
“Ningeshauri tu mamlaka zinazohusika, zikiwemo za utumishi na utawala bora zifuatilie suala hili, maana ni kashfa kubwa kwa Serikali ambayo tunaiamini kwamba inawajali wananchi, wakiwemo watumishi wake.”
Mkurugenzi hajui
Gazeti hili lilimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Peter Ngusa, ambaye alisema hana taarifa kwamba kuna watendaji wa vijiji ambao ni ‘vibarua’.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, Juma Mbegu Mohammed Kizwezwe ambaye ni Diwani wa Kata ya Msanga, alipotafutwa na mwandishi wetu na kuelezwa kuhusu taarifa hizo aliguna na kukata simu, na alipotafutwa kwa mara ya tatu alisema yuko ‘busy’ angepiga mwenyewe simu, jambo ambalo hakulifanya hadi gazeti hili linaingia mtamboni.
Jitihada za kumpata Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angela Kairuki, kwa ajili ya ufafanuzi zaidi hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni.
Majukumu yao
Kulingana na Kanuni za Utumishi wa Umma, majukumu ya kazi ya Mtendaji wa Kijiji ni pamoja na kuwa ndiye Ofisa Masuuli na Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Kijiji, Kusimamia Ulinzi na Usalama wa raia na mali zao na kuwa Mlinzi wa Amani na msimamizi wa Utawala Bora katika kijiji, Kuratibu na kusimamia upangaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kijiji, Kuratibu mikutano na kamati zote za Halmashauri ya Kijiji, na Kutafsiri na kusimamia sera, sheria na taratibu za uendeshaji wa Serikali ya Kijiji.
Majukumu mengine ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji ambaye anawajibika kwa Ofisa Mtendaji wa Kata, ni Kuandaa taarifa za utekelezaji wa kazi katika eneo lake na kuhamasisha wananchi katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya kuondoa njaa, umaskini na kuongeza uzalishaji maji, Yeye ndiye kiongozi wa wakuu wa vitengo vya kitaalam katika kijiji, Kusimamia, kusikiliza, kutatua malalamiko na migogoro ya wananchi, na Kusimamia utungaji wa sheria ndogo za kijiji.
Kanuni zinasemaje?
Kwa mujibu wa Sheria za Kazi, watendaji hao walistahili kuthibitishwa kwenye ajira na kuwa katika Daraja la Tatu ambapo kiwango chao cha mshahara kinapaswa kuwa katika Ngazi ya TGS B.
Tamko namba 1 hadi 7 la Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 linatoa tafsiri ya Utumishi wa Umma, misingi na malengo ya Utumishi wa Umma na maadili ya msingi ya uwepo wa Utumishi wa Umma.
Toleo la Tatu la Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 zinatoa ufafanuzi wa masuala ajira, uteuzi, nidhamu, kuthibitisha kazini watumishi, likizo, matibabu, mafunzo, mitihani, posho mbalimbali, mikopo ya watumishi, nyumba na samani na uendeshaji wa jumla wa Utumishi wa Umma.
Lakini pia Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 ambazo zimetungwa chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 zinaeleza masuala ya msingi yanayohusu ajira au uteuzi wa watumishi wa umma, kuthibitishwa kazini; tathmini ya utendaji kazi; kupandishwa cheo; kusitishwa kwa ajira; nidhamu; rufaa; kanuni za maadili za watumishi wa umma; na mafao ya kustaafu.
Kulingana na Sheria na Kanuni mbalimbali za Utumishi wa Umma, mtumishi ana wajibu wa kutumia elimu, ujuzi na bidii katika kutoa huduma bora kwa wananchi. Kadhalika ana haki na stahiki mbalimbali anazopaswa kuzipata kutoka kwa mwajiri.
Haki hizi ni pamoja na Kupewa Mkataba wa Kazi (Barua ya Ajira) unaoonyesha jina la mtumishi, anuani yake, tarehe ya ajira, aina ya ajira, cheo, ngazi ya mshahara, kiwango cha mshahara na masharti mengine ya ajira kama yanavyoainishwa kwenye Kanuni D.32 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009.
Watendaji hawa wa vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe walipaswa kuthibitishwa kazini baada ya kipindi cha majaribio kisichozidi miezi kumi na mbili (12) ambacho lengo lake ni kupima tabia na utendaji wao wa kazi.
Aidha, miezi mitatu (3) kabla ya muda wa majaribio kuisha, msimamizi wa kazi anapaswa kuamua kama: mtumishi huyo athibitishwe kazini, au; aongezewe muda wa majaribio, au; ajira yake isitishwe.
Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (1) na (2) (a), (b) na (c) ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 na Kanuni D.40 na D.43 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma, 2009.