PIRAEUS, Ugiriki
TIMU ya Manchester City, imetwaa taji lake la kwanza la UEFA Super Cup chini ya Kocha, Pep Guardiola kwa mikwaju ya penalti mbele ya Sevilla baada ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini hapa.
Ikitoka kupoteza Ngao ya Jamii kwa kufungwa na Arsenal kwa mikwaju ya penalti siku 10 zilizopita, timu hiyo iliyotwaa mataji matatu msimu uliopita nusura sherehe zao ziendelee kutiwa doa kutokana na ushindani waliopata kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi ya Europa.
Mchezaji Youssef En-Nesyri, aliifungia Sevilla bao la kuongoza lakini City ilisawazisha kupitia kwa Cole Palmer kwa kichwa na kufanya mchezo huo wa Super Cup kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.
Mikwaju tisa ya kwanza yote iliingia kambani kabla ya Nemanja Gudelj kupiga na kugonga mtamba wa panya na kuifanya Man City iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kuibuka na ushindi wa penalti 5-4.
Guardiola ambaye ni raia wa Hispania, anakuwa kocha wa kwanza wa taifa hilo kutwaa taji la UEFA Super Cup akiwa na timu tatu tofauti akifikia rekodi ya Carlo Ancelotti aliyetwaa mara nne.
Pia City inakuwa timu ya sita kutwaa taji hilo.