‘Mama Asemewe’ yahamasisha vijana Singida kumpigia kura Dkt. Samia

Na Mwandishi Wetu, Singida

MWENYEKITI wa Kampeni ya Mama Asemewe Taifa, Geofrey Kiliba, ameendelea na ziara yake mkoani Singida ambapo, amekutana na vijana maafisa usafirishaji katika Wilaya ya Manyoni na kuwahamasisha kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa mikakati ya kampeni inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jamii katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pamoja na kulinda amani na utulivu wa Taifa la Tanzania.

Katika mazungumzo yake na vijana hao, Kiliba amewasisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, hususani katika kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa vijana ndiyo nguvu kuu ya Taifa na wana nafasi ya kipekee katika kuleta mabadiliko chanya kwa mustakabali wa Tanzania.

Aidha, amehimiza vijana kuendelea kudumisha mshikamano, umoja na amani, akisisitiza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mafanikio hayo.

Ziara hiyo imeendelea kutoa hamasa kubwa kwa wananchi wa Singida, ambapo kampeni ya Mama Asemewe inatarajia kuendelea na mikutano na vikao vya uhamasishaji katika mikoa mingine kuelekea uchaguzi mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *